Jumatano, 18 Desemba 2013

MWANAFUNZI AUAWA KWA KUKATWA KOROMEO SINGIDA

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na tukio la Mwanafunzi kukatwa Koromeo.
MWANAFUNZI wa Darasa la kwanza katika shule ya msingi kijiji cha Tatu kata ya Kiomboi tarafa ya Kisiriri wilaya ya Iramba Mkoa wa Singida,Geofrey Emmanuel (9) amefariki dunia baada ya kukatwa koromeo kwa kisu na kusababisha kuvunja damu nyingi.
Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo alichinjwa kinyama na Francis Lukumbitio (30) mkazi wa kijiji cha Kizenga ambaye naye aliuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kumwagiwa Petroli na kisha kuwashwa moto.
Kamanda wa Mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela amesema tukio hilo la kusikitisha limetokea Desemba 15 mwaka huu saa 10.00 jioni katika kijiji cha Tatu kata ya Kiomboi wilaya ya Iramba.
Amesema siku ya tukio mwanafunzi huyo akiwa anachunga mbuzi pamoja na watoto wenzake ghafla alitokea Francis akiwa amebeba kisu mkononi na kumshika kwa nguvu na kuanza kumkokota hadi kichakani na kisha kutekeleza unyama wake huo.
Akifafanua zaidi, amesema wenzake waliweza kufuatilia na walipofika eneo la tukio walikuta mwanafunzi huyo tayari amekwishafariki dunia kutokana na kukatwa koromeo.
“Watoto hao baada ya kuona tukio hilo, walitoa taarifa kijijini na haraka wananchi waliweza kukusanyika na kumfuata mtuhumiwa kijijini kwake Kizega na walifanikiwa kumkuta Francis akiwa nuyumbani kwake Walimtoa nje na kuanza kumpiga kwa fimbo, marungu na mawe na alipokuwa taabani walimwagia petroli na kumwasha moto”,amesema Kamwela.
Kamanda Kamwela amesema wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na mauaji hayo ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wawafikishe watuhumiwa kwenye vyombo vya dola ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
 

SAFARI YA MWISHO YA NELSON MANDELA, AZIKWA KIJIJINI KWAO

Jeneza la Mzee Nelson Mandela likisindikizwa na kikosi cha Jeshi katika mazishi ya Kitaifa yaliyohudhuriwa na watu mashuhuri Duniani Bill Clinton, Oprah, Prince Charles, Richard Branson na wengine wengi.
 Maafisa wa Jeshi nchini Afrika Kusini.
 Mjane wa Marehemu Mzee Nelson Mandela Graca Machel akitafakari maisha ya upweke, na picha hii hapa chini ni mama Winnie Mandela katika majonzi mazito siku ya mazishi ya mwana Africa Nelson Mandela

Alhamisi, 12 Desemba 2013

JESHI LA POLISI LAUA MAJAMBAZI WAWILI

Kamanda wa polisi mkoa wa Singida,SACP Geofrey Kamwela,akionyesha bunduki ya kijeshi aina ya SMG no.34555  iliyokuwa ikitumiwa na watu wawili wanaodhaniwa kuwa majamabazi katika kijiji cha Manga manispaa ya Singida.
 JESHI  la Polisi mkoani Singida limewauwa watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakati wa kurushiana rasasi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, SACP, Geofrey Kamwela amesema tukio hilo limetokea desemba tisa mwaka huu saa 12:00 jioni, huko katika kijiji cha Manga nje kidogo ya mji wa Singida.
Amesema watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na bunduki moja ya kijeshi aina ya SMG, walifika kijijini hapo kwa lengo la kufanya uhalifu.
Kamanda Kamwela, amesema watu hao ambao miili yao imehifadhi kwenye chumba cha mochwari katika hospitali ya mkoa, majina na makazi yao bado hayajajulikana.
Akifafanua, amesema taarifa za siri kutoka kwa raia wema zilifikia jeshi la polisi na ndipo askari polisi walipofika kwenye eneo la tukio.
“Baada ya polisi kufika kijijini hapo watu hao walistuka kuwa wanafuatilwa na askari polisi na hivyo kuanza kukimbia kuelekea kijiji cha Uhamaka kwa kutumia pikipiki yenye namba za usajili T. 634 BTW aina ya Sanlag yenye rangi nyeusi”,amesema Kamwela.
Amesema walipoona Polisi wanawakaribia waliamua kutelekeza pikipiki yao hiyo na kuanza kukimbilia porini kwa miguu.
“Hali ilipokuwa ngumu zaidi, walianza kuwarushia polisi risasi, hivyo polisi nao ikwabidi kujibu mapigo.  Katika majibizao hayo ya risasi, majambazi mawili yaliweza kujeruhiwa huku mmoja akifanikiwa kutoroka”
Amesema majambazi hayo yaliyojeruhiwa yalifariki dunia wakati yanakimbizwa katika hospitali ya mkoa kwa matibabu,lakini yakafia njiani.
Amesema katika eneo la tukio, ilipatikana bunduki moja aina ya SMG yenye namba 34555 ikiwa na risasi saba kwenye magazine.  Pia pikipiki iliyokuwa iantumiwa na majambazi hayo, iliwezea kupatikana.
Kamwela alitoa wito kwamba wananchi waendelee na moyo huo huo wa kuwafichua watu wanaowatilia shaka ili waweze kudhibitiwa mapema kabla ya kufanya uhalifu.



RAIS JAKAYA KIKWETE AHUDHURIA SHEREHE ZA MIAKA 50 UHURU WA KENYA

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete(kulia) wakihudhuria sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Kenya zilizofanyika katika uwanja wa Michezo wa Kasarani mjini Nairobi leo.Kushoto ni Mwenyeji Rais Wa Kenya Uhuru Kenyatta.Watatu kushoto ni Naibu Rais Wa Kenya William Ruto,Watano Kushoto ni Waziri Mkuu wa Ethiopia Haile Mariam Desalegn, na Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi na mkewe
Ushirikiano na umoja katika matukio muhimu kama haya, jambo jema sana kufanywa na kiongozi mkuu wa Nchi, katika hali ya kawaida tungeweza kusema amechoka baada ya majuzi tu kumaliza sherehe za uhuru wa Tanganyika na kisha kwenda katika ibada maalumu ya Hayati Mandela. tunahitaji ushirikiano na umoja huo hudumu

 

AJALI MBAYA YATOKEA NA KUPOTEZA MAISHA YA WATU 12

Ajali mbaya imetokea leo hii, na yasemekana watu wapatao 12 wamepoteza maisha hapo hapo mara baada ya ajali kutokea, ajali hiyo imetokea maeneo ya Kabuku mkoani Arusha, gari iliyohusika na ajali hiyo ni basi la Burdani lililokuwa linatoka Korogwe kwenda Arusha. taarifa zaidi tutakujuza mapema iwezekanavyo mara baada ya kuletewa na mwakilishi wetu aliyeko huko, na taarifa rasmi kutoka jeshi la polisi juu ya idadi kamili ya waliopoteza maisha, idadi hiyo ya watu 12 ni taarifa zilizotumwa mara tu baada ya ajali, Mungu awajalie afya njema wale wote waliopatwa na ajali hiyo, awape faraja ya pekee wakati huu ambao ni mgumu sana kwako

BUNGE LIMEPITISHA AZIMIO KUWATAKA MAWAZIRI TAMISEMI WAJIPIME

Dodoma.Bunge limepitisha azimio la kuwataka mawaziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kujipima iwapo wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo nyeti.
Azimio hilo lilipitishwa jana na wabunge kwa kura ya ndiyo bila kupingwa, baada ya kuhojiwa na Spika wa Bunge Anne Makinda iwapo wanaipokea taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Laac) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake Rajabu Mbaruku.
Moja ya mapendekezo yake ni Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia na manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kujipima kama wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo kutokana na kugubikwa na vitendo vya ufisadi.
Kwa mujibu wa taratibu za Bunge, taarifa ya kamati inapowasilishwa na kupitishwa pamoja na mapendekezo yake, huwa ni azimio kamili ambapo Serikali hutakiwa kutoa maelezo ya utekelezaji wake.
Kabla ya azimio hilo kupitishwa, Mwenyekiti wa Laac, Rajabu Mbaruku alijibu michango ya wabunge waliochangia katika taarifa ya kamati yake iliyowasilishwa Ijumaa iliyopita, akiwemo Waziri Ghasia.
Akizungumza baadaye, Mbaruku alisema hayo ndiyo mapendekezo na Serikali itatakiwa kuyatolea maelezo ya jinsi yatakavyotekelezwa. “Hata waziri mkuu nimemtaja kwa jina, na nimesisitiza kama ananisikia kuhusu ofisi yake,” alisema.
Katika mchango wake, Waziri Ghasia alijaribu kupangua tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa katika wizara yake ikiwamo kuwapo ufisadi, ubadhirifu na mtandao wa wizi unaohusisha Hazina, Wizara na Halmashauri.
Ghasia alikiri Halmashauri ya Mbarali ilitumiwa fedha kuliko kiwango kilichoidhinishwa na Bunge na kwamba
suala la halmashauri mbili za Tanga kupewa zaidi ya Sh2 bilioni haikuwa sahihi bali yalikuwa ni makosa ya Mkaguzi Mkuu wa Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kuhusu ufisadi wa zaidi ya Sh600 milioni zilizotolewa na wafadhili kwa ajili ya mpango wa maboresho ya Serikali za Mitaa, alisema haamini kama maneno yaliyonukuliwa na vyombo vya habari kuhusu fedha hizo yalisemwa na wafadhili.
Wafadhili wa mradi huo walinukuliwa wakilalamikia ufisadi huo na kudai kwa sasa hawana la kufanya na wanamwachia Rais, huku wakieleza kushangazwa na Rais kuteua watu dhaifu kuendesha wizara nyeti kama Tamisemi.
Kuhusu hilo, Ghasia alisema hadhani maneno hayo ni ya wafadhili akisema ni majungu, ni maneno ya waandishi kwa sababu huwa wanatafuta mambo yanayogusa jambo fulani ili kuuza magazeti.
Hata hivyo, Ghasia alikiri kwamba ulifanyika ukaguzi na yalibainika matumizi ambayo hayakufuata taratibu na kusisitiza kuwa fedha zilizotumika bila kufuata taratibu zilikuwa Sh444.8 milioni na siyo Sh600 milioni.
Alisema kuwa tuhuma kwamba anawalinda watuhumiwa wa ufisadi na kuwahamisha wale wanaotuhumiwa si za kweli kwani wizara imekuwa ikichukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi hao na hata kuwafikisha kortini.
Alitolea mfano wa Halmashauri ya Kishapu ambayo watumishi 14 wamesimamishwa kazi na masuala yao hivi sasa yanashughulikiwa na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Ofisi ya Takukuru.
Pamoja na maelezo ya Waziri Ghasia, bado Mwenyekiti wa Kamati alisisitiza kuwapo matatizo makubwa
Tamisemi na ndipo alipowataka Ghasia na Manaibu wake kujipima wenyewe kama bado wanafaa kuongoza wizara hiyo nyeti.
Mwenyekiti huyo alisema si kweli kama alivyosema Waziri Ghasia kuwa hakuna mtandao wa ufisadi na
kusisitiza kuwa fedha zilizopelekwa jijini Tanga hazikurudishwa Hazina na badala yake zilitumiwa na Halmashauri hiyo.
Alisema kinachoonekana ni kwamba ulikuwapo mpango wa kuzipeleka fedha kwenye baadhi ya Halmashauri nje ya fedha zilizoidhinishwa lakini baadaye fedha hurudishwa kwa wanamtandao huo baada ya kutakatishwa.
Mwenyekiti huyo alisema Halmashauri zinazopelekewa fedha hizo zilizo nje ya bajeti, hupelekewa fedha hizo kwa malengo ya kuzitakatisha kisha kuzirejesha Hazina ambapo wahusika hunufaika nazo.
Ijumaa wakati akiwasilisha taarifa ya kamati, kamati hiyo iliilipua Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikiituhumu kuwa sehemu ya mtandao wa ufisadi serikalini.
Alisema bado kuna ubadhirifu, ufisadi na utovu wa nidhamu wa hali ya juu wa matumizi ya fedha za umma kutokana na Tamisemi kutosimamia au yenyewe kuhusika moja kwa moja na ufisadi huo.
Mfano wa mwaka 2011/2012 ambapo Sh1.6 bilioni zilitumika nje ya bajeti iliyoidhinishwa katika halmashauri 38 na Sh2.6 bilioni zilihamishwa kutoka akaunti moja kwenda nyingine bila kurudishwa.

Kamati hiyo imebaini kwamba upo mtindo wa Serikali kutuma kwa Halmashauri kiasi kikubwa cha fedha kuliko kiasi cha fedha kilichoidhinishwa na Bunge katika fungu husika wakati wa upitishaji wa bajeti.
Kamati hiyo imetolea mfano wa Sh2 bilioni zilizotumwa Halmashauri ya Jiji la Tanga na Sh500 milioni zilizotumwa Halmashauri ya Mji wa Korogwe zikiwa zaidi ya kiasi kilichokuwa kimeidhinishwa na Bunge.
“Kitendo hiki ambacho kinafanyika kwa ushirikiano wa hali ya juu wa Hazina,Tamisemi na Halmashauri kinaashiria kuwapo mtandao wa kutisha wa kifisadi baina ya mamlaka hizo,” alisema.
Kamati hiyo imeituhumu pia Tamisemi inayoongozwa na Waziri Hawa Ghasia, kuwahamisha haraka watumishi wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu kutoka halmashauri moja kwenda nyingine.
“Kamati imebaini kwamba Tamisemi imekuwa ikitumia mtindo huu kuwalinda watumishi mafisadi ndani ya halmashauri na kuifanya kamati iamini Tamisemi ni sehemu ya mtandao huu,” imesema.
Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema kwa makusudi mazima, Tamisemi imekuwa ikieneza saratani hiyo ya ufisadi kwenye halmashauri nyingi iwezekanavyo na kuitaka Serikali kuachana na mtindo huo.
Ubadhirifu Wakurugenzi 70
Itakumbukwa Agosti 19 mwaka huu, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ilitoa taarifa yake baada ya kubaini kuwepo kwa mtandao wa ufisadi unaoshirikisha Wakurugenzi 70 wa Halmashauri mbalimbali hapa nchini ambao wanashirikiana na baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kitengo cha Hazina.
Baadhi ya halmashauri hizo ni pamoja na Wilaya ya Monduli, Arusha, Mwanza, Mbeya na Ilala.
Ilielezwa kuwa Tanzania Bara ina halmashauri 134, kwa hiyo ina maana zaidi ya nusu ya wakurugenzi wanajihusisha na mambo hayo.
“Baadhi ya wakurugenzi hao walihamishwa kwenye vituo vyao vya kazi kutokana na kashfa ya matumizi mabaya
ya fedha za Serikali, lakini bado wanajihusisha na mambo haya,” alisema Mbarouk alipokuwa akiwasilisha taarifa yake kwa waandishi wa habari.

“Kuna zaidi ya Wakurugenzi 70 wako kwenye mtandao wa ufisadi kwa kushirikiana na watendaji wa Hazina na Tamisemi, jambo ambalo limesababisha halmashauri zao kupata hati chafu kwa miaka mitano mfululizo,” alisema Mbarouk.
Aliongeza wakurugenzi hao wamekuwa wakishirikiana na wahasibu wao katika kutumia vibaya fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri zao.
Akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe ambaye halmashauri yake ilifanya vibaya katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini hajachukuliwa hatua na badala yake amehamishwa kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.

WAATHIRIWA WA UKIMWI WAISHI MAISHA MAREFU

Mtu anapogundua kwa mara ya kwanza kwamba ameambukizwa virusi vya HIV hupatwa na mshtuko. Wengine huona kifo kimepiga hodi, wanahofia kumweleza yeyote kutokana na unyanyapaa. Lakini leo hii hali imebadilika. Kuna matumaini. Dorothy Onyango ambaye ni muathirika wa HIV kutoka Kenya.Dorothy pia  ni mwenyekiti wa shirika la kina mama wanaoishi na ukimwi nchini Kenya liitwalo WOFAK.
Anaelezea kuwa maendeleo makubwa yamefikiwa kuwapa waathiriwa matumaini na kwamba hivi leo kuna majaribio ya dawa mpya na chanjo. Hizi ni miongoni mwa habari njema kwa waathiriwa na wasio waathiriwa. Anasema ana matumaini kuwa kizazi kisicho na ukimwi chawezekana.
Mama huyo anasema kinyume na ilivyokuwa miaka ya themanini na tisini, waathiriwa wa Ukimwi  sasa wamepata sauti. Wamepata dawa za kudhibiti gonjwa hilo na wanajua namna ya kujitunza na wanaishi  maisha marefu kama watu wengine wowote.
Ni kitu cha kawaida kwa muathiriwa kupatwa na mshtuko mara anapogundua ameambukizwa virusi vya HIV au Ukimwi. Dorothy ambaye ameishi na virusi hivyo kwa zaidi ya miaka 15 anaeleza  kuwa aligunduliwa kuwa na virusi hivyo mapema miaka ya ‘90 wakati huko Kenya mabango makubwa ya watu waliokondeana kwa ukimwi yakiezekwa barabarani na vyombo vya habari kutahadharisha kuhusu gonjwa hilo. Hakumweleza yeyote  kuwa ana virusi vya HIV hadi baada ya miaka mitano.
Nilitaka kujua kimya cha Dorothy cha  miaka mitano baada ya kugunduliwa na HIV aliweza kumudu vipi maisha. Je, alikula chakula cha aina gani au alikuwa na msukumo wa aina gani binafsi kuweza kuishi na kuficha ukweli juu ya hali yake  bila kuonekana kuwa muathiriwa?

Mama huyo anasema alikwenda kimya kimya kwenye mikutano ya waathirwa, na kusoma kila habari zilizoandikwa kuhusu ukiwmi. Alikula vyema na kujitunza. Na huko Kenya dawa ya Kemron iliyotangazwa kuwa inaweza kudhibiti maradhi hayo aliitumia. Alitumia pia dawa nyingine kwa jina Pearl Omega. Lakini baadaye akaamua kuzungumza na wakenya waliokuwa wamejitokeza wazi kueleza  kuwa ni waathiriwa na hivyo kupata msaada wa kimawazo na madawa.
Na kwa wale wanaogunduliwa na HIV na Ukimwi na kutangaza vita vya kusambaza virusi hivyo kwa wengine. Dorothy anawashauri wajilinde wenywe. Anatahadharisha  kuwa wanaweza kudhoofisha afya yao zaidi kwa kupata maambukizo mengine ya zinaa na kukaribisha mauti kabla ya wakati wao.

Anasema mtu akiwa muathirika hakuna njia ya kubadili hali yake kuwa si muathirika, na kwamba kilicho bora kufanya ni kutafuta msaada kuweza kuishi maisha marefu kwa kutumia madwa na kula vizuri. Dorothy ambaye amekuwa mwenyekiti wa chama cha wanawake wanaosihi na ukimwi nchini Kenya kinachojulikana kwa kifupi kama WOFAK, anawapa matumaini waathiriwa wa HIV na Ukimwi na anaandika kitabu kuhusu maisha yake na wanawake wengine walioathiriwa lakini wanaoishi maisha ya kawaida.
Na kwa hakika ikiwa wewe ni muathiriwa au una mtu aliyeathirika na virusi vya HIV na Ukimwi fahamu kwamba yapo  matumaini na mifano dunia hii na haswa Afrika ni chungu nzima. Ishi kwa matumaini.

HESHIMA ZA MWISHO ZAANZA KUTOLEWA KWA MANDELA

Waombolezaji nchini Afrika Kusini wanaingia siku ya pili katika zoezi la kutoa heshima za mwisho kwenye mwili wa Rais wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela.
Maelfu ya watu wamejipanga kwenye mistari wakisubiri kutoa heshima zao za mwisho kwenye mwili huo uliolazwa katika ikulu kwenye jengo la Muungano mjini Pretoria.
 
Mjane wa Marehemu Graca Machel na Rais wa sasa wa Afrika Kusini Jacob Zuma, viongozi wa serikali na wanafamilia walikuwa ni miongoni mwa waliotoa heshima zao za mwisho kwenye mwili wa Marehemu Mandela siku ya jumatano.
Viongozi mbali mbali pamoja na raia wa Afrika Kusini walianza kutoa heshima zao za mwisho kuanzia jumatano
Kabla ya kuwekwa katika jengo la ikulu awali mwili huo ulichukuliwa katika msafara kutoka chumba cha maiti cha hosptali hadi kwenye jengo la Muungano.
Msafara wenye jeneza la Marehemu uliondoka mjini katika Hosptali ya jeshi muda mfupi siku ya jumatano. Jeneza lilibebwa kwenye gari maalum na kufunikwa bendera ya Afrika Kusini.
Wananchi walijipanga kando kando ya barabara lilipopitishwa jeneza kama ishara ya kutoa heshma za mwisho kwa mwili wa marehemu.
Msafara ulipita katika mitaa huku baadhi ya raia wakikimbia pembeni kwenye mstari wa askari wa wanajeshi
Wanajeshi waliobeba jeneza hilo walisonga hatua kwa hatua hadi katika Majengo ya Muungano eneo alikoapishwa kuwa rais wa kwanza mzalendo wa Afrika kusini 1994.
Marehemu Mandela atazikwa nyumbani kwake katika kijiji Qunu katika jimbo la Cape Mashariki siku ya jumapili.

Ijumaa, 6 Desemba 2013

KIFO CHA NELSON MANDELA CHALETA GUMZO DUNIANI

Wananchi wamejitokeza katika sehemu nyingi za Afrika Kusini wakiomboleza kifo cha kiongozi wao Nelson Mandela Mandela.
Mji wa Johannesburg umemiminika watu waliojitokeza kumkumbuka Mandela na kutoa rambi rambi zao kwa jamii, familia na marafiki wao.
Viongozi duniani pia wameendelea kutuma rambirambi zao kufuatia kifo cha Mandela.
Kifo cha Mandela kilitangazwa hapo jana Alhamisi saa za usiku naye Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma aliyesema kuwa Afrika Kusini inaomboleza kumpoteza kiongozi huyo waliyemuenzi sana kama mtoto wao , baba yao na kiongozi wa taifa hilo.
Mandela alifariki nyumbani kwake mjini Johanesburg na alikuwa ameugua homa ya mapau kwa muda mrefu.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa Mzee Mandela, miongoni mwa wengine kama Oliver Tambo, Govan Mbeki na wengine, walijitolea maisha yao na ujana wao wote katika kupigania haki na kuikomboa Afrika Kusini. Walijivunia kweli walichoamini na wakatekeleza. Sasa ni jukumu letu na wadogo wetu kuendeleza kazi ya Mandela.''
Rais wa Malawi Joyce Banda, "Wakati kama huu, sote tumepata mshtuko. Sio kuwa hatukujua kitatokea, lakini ni huzuni kwa tulichopoteza. Ningependa kuelezea masikitiko yangu kwa kumpoteza kijana wa Afrika Dr. Nelson Mandela kwasababu vita alivyopigana sio tu dhidi ya ubaguzi wa rangi bali ni vita dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote dhidi ya binadamu.
Na ndio maana vijana, na wazee, wake kwa waume, weupe na weusi tajiri na masikini wote wamejihusisha na yeye na vitu alivyopigania."
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema kuwa Hayati Nelson Mandela atazikwa tarehe kumi na tano Jumapili mwezi Disemba katika eneo la Qunu mkoa wa Estern Cape.
Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, "Kifo cha mandela. Huyu alikuwa mwakilishi wa utu duniani.
Pia amekuwa chanzo cha matumaini kwa wengine wengi ambao wanakabiliana na unyanyasaji na kunyimwa haki, hata miaka yote hiyo baada ya kuwakomboa watu wake wenyewe.
Katika ulimwengu uliogubikwa na migawanyiko, amekuwa mfano mwema wa utangamano na sioni uwezekano wa kupatikana mwingine kama yeye katika miaka mingi ijayo."

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, ametangaza siku tatu za maombolezi, kufuatia kifo cha mzee Nelsomn Mandela, akisema kua Afrika na dunia nzima kwa ujumla imempoteza shujaa mkubwa sana katika karne ya 20 na 21.
Kikwete alisema kupitia taarifa kwa vyombo vya habari kua Mandela ni kiongozi wa kipekee na mtu aliyeenziwa sana na dunia nzima pamoja na watu wa Afrika Kusini baada ya kupigania sana demokrasia nchini Afrika Kusin
Kikwete alisema mfano wa Mandela unapaswa kuigwa na watu wote duniani .
Kwa upande wake Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, amesema kuwa Mandela alikuwa mfano mzuri wa umuhimu wa kuwa na matumaini na kuwataka watu kuwa na uelewa wa kuwasamehe bila masharti wale wote wanaotukuosea.
Naye Rais wa Rwanda Paul Kagame,amesema kua Mandela ataendelea kuishi kwenye mioyo ya wengi wetu.
Naye Rais mstaafu Daniel Moi ambaye alikuwa madarakani wakati Mandela alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, amempongeza Mandela kwa kuhakikisha utulivu wa kisiasa barani Afrika na kuwa mfano bora kwa viongozi wengine.
Naye Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amesema kuwa Mzee Mandela, pamoja na washirika wake, Albert Luthuli, Walter Sisulu, Govan Mbeki, Oliver Thambo na wengine wengi,walijitolea maisha yao kuleta demokrasia nchini Afrika Kusini.
Walifanya kila walichoweza kuhakikisha kwa wanawakomboa watu wa taifa lao.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Museveni amesema ni jukumu la vijana sasa kuiga mfano wa Mandela kuhakikisha kuwa Afrika inalindwa dhidi ya ukoloni mambo leo na kutengwa.

Jumatatu, 2 Desemba 2013

WANAOTOA HUDUMA KWA KUTOZA WATU PESA NI MATAPELI

Katika ibada ya jumapili, ujumbe wa Neno la Mungu kutoka katika kanisa la Bethel Assemblies of God, linaloongozwa na Mchungaji kiongozi James Kalaghe lililopo Bunju “B” ulikuwa ni; Mguso wa kimungu katika kanisa lililo najisika, ujumbe huu ulihubiri na Mchungaji Milanzi
katika mahubiri ibadani hapo, mchungaji huyo alisema, Kanisa nyakati hizi tulizo nazo leo, limetiwa unajisi, nyakati zile za Yesu palikuwepo na mwanamke mmoja ambaye alikuwa na tatizo la kutokwa na damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, kwa nyakati zile yule mwanamke alikuwa ni najisi sana, na watu walikuwa wakijiepusha kuwa naye karibu, kwahiyo alitengwa na watu kila alipokwenda. Lakini siku moja alisikia habari za Yesu, na akachukua hatua ya kwenda kwa Yesu akisema moyoni mwake, nikigusa vazi lake nitapona.
Jinsi alivyokuwa yule mwanamke katika hali ya unajisi wake, ndivyo lilivyo kanisa la leo, kanisa limejaa unajisi, wahubiri na wachungaji wanaofanya maombezi kwa kuwatoza watu pesa, maombezi hayo ni batili “nifeki” hao ni matapeli wakawaida. Waimbaji wa nyimbo za Injili wanaotoa huduma kwa kuomba malipo ya ile huduma hao pia ni matapeli wakubwa na aibu yao inakuja
Matendo hayo ndiyo yamelitia kanisa unajisa na kanisa linanuka! Na katika ulimwengu wa roho kanisa linavyo onekana mbele za Mungu ni wakati ule yule mwanamke aliyetokwa damu alivyokuwa akitengwa na wanadamu kutokana na unajisi aliokuwa nao, ndivyo na kanisa la sasa linavyo tengwa na Mungu kutokana na unajisi huu.
Mchungaji aliwataka waumini wa kanisa la Bethel Assemblies Of God watubu kwaniaba ya kanisa la Tanzania ili Mungu alitakasa kanisa kwa kuliponya na kuondoa unajisi

MILIONI 346 ZAPATIKANA KWENYE HARAMBEE YA KUCHANGIA UJENZI WA HOSPITALI TANGA


Jumla ya shilingi milioni 346 zimepatikana katika hafla ya uchangiaji ujenzi wa hospitali ya Mtakatifu Raphael inayomilikiwa na kanisa Anglikana,wilayani Korogwe mkoani Tanga. Hafla hiyo iliongozwa na askofu Valentino Mokiwa wa jimbo kuu la Dar es salaam kanisa Anglikana huku mgeni rasmi akiwa mkuu wa mkoa wa Tanga aliyemwakilisha waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa Mizengo Pinda aliyeshindwa kufika katika hafla hiyo.

Pamoja nao pia viongozi wengine wa serikali akiwemo mkuu wa wilaya ya Korogwe Mrisho Gambo pamoja na wananchi na waumini wa kanisa hilo walihudhuria katika hafla hiyo.
 Kwa hakika kazi hii imekuwa njema sana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na kanisa kwa ujumla wake, Askofu Mokiwa aliwashukuru wale wote waliotoa michango yao kwa lengo la kufanikisha huduma hiyo muhimu kwa jamii, pia aliwaombea baraka wale wote walionyesha moyo wa kutoa mali zao

Alhamisi, 24 Oktoba 2013

NMB YATOA MSAADA HOSPITALI YA ILEJE MBEYA

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Janet Mbene akishukuru uongozi wa benki ya NMB kwa msaada wa mashuka na vitanda vya akina mama katika  hospitali ya Itumba  wilaya ya Ileje .Msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni Tano umetolewa na benki ya NMB kupitia tawi la Ileje mwishoni mwa wiki katika viwanja vya hospitali ya Itumba.
 Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ileje, Nd. Mohamed Mwala akimshukuru Meneja wa Kitengo cha Huduma za Serikali  wa NMB , Bw. Elieza Msuya  baada ya kupokea msaada wa vitanda na mashuka ya hospitali ya wilaya ya vilivyotolewa na benki ya NMB.  Anayeshuhudia makabidhiano hayo ni Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Janet Mbene

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595