Alhamisi, 12 Desemba 2013

WAATHIRIWA WA UKIMWI WAISHI MAISHA MAREFU

Mtu anapogundua kwa mara ya kwanza kwamba ameambukizwa virusi vya HIV hupatwa na mshtuko. Wengine huona kifo kimepiga hodi, wanahofia kumweleza yeyote kutokana na unyanyapaa. Lakini leo hii hali imebadilika. Kuna matumaini. Dorothy Onyango ambaye ni muathirika wa HIV kutoka Kenya.Dorothy pia  ni mwenyekiti wa shirika la kina mama wanaoishi na ukimwi nchini Kenya liitwalo WOFAK.
Anaelezea kuwa maendeleo makubwa yamefikiwa kuwapa waathiriwa matumaini na kwamba hivi leo kuna majaribio ya dawa mpya na chanjo. Hizi ni miongoni mwa habari njema kwa waathiriwa na wasio waathiriwa. Anasema ana matumaini kuwa kizazi kisicho na ukimwi chawezekana.
Mama huyo anasema kinyume na ilivyokuwa miaka ya themanini na tisini, waathiriwa wa Ukimwi  sasa wamepata sauti. Wamepata dawa za kudhibiti gonjwa hilo na wanajua namna ya kujitunza na wanaishi  maisha marefu kama watu wengine wowote.
Ni kitu cha kawaida kwa muathiriwa kupatwa na mshtuko mara anapogundua ameambukizwa virusi vya HIV au Ukimwi. Dorothy ambaye ameishi na virusi hivyo kwa zaidi ya miaka 15 anaeleza  kuwa aligunduliwa kuwa na virusi hivyo mapema miaka ya ‘90 wakati huko Kenya mabango makubwa ya watu waliokondeana kwa ukimwi yakiezekwa barabarani na vyombo vya habari kutahadharisha kuhusu gonjwa hilo. Hakumweleza yeyote  kuwa ana virusi vya HIV hadi baada ya miaka mitano.
Nilitaka kujua kimya cha Dorothy cha  miaka mitano baada ya kugunduliwa na HIV aliweza kumudu vipi maisha. Je, alikula chakula cha aina gani au alikuwa na msukumo wa aina gani binafsi kuweza kuishi na kuficha ukweli juu ya hali yake  bila kuonekana kuwa muathiriwa?

Mama huyo anasema alikwenda kimya kimya kwenye mikutano ya waathirwa, na kusoma kila habari zilizoandikwa kuhusu ukiwmi. Alikula vyema na kujitunza. Na huko Kenya dawa ya Kemron iliyotangazwa kuwa inaweza kudhibiti maradhi hayo aliitumia. Alitumia pia dawa nyingine kwa jina Pearl Omega. Lakini baadaye akaamua kuzungumza na wakenya waliokuwa wamejitokeza wazi kueleza  kuwa ni waathiriwa na hivyo kupata msaada wa kimawazo na madawa.
Na kwa wale wanaogunduliwa na HIV na Ukimwi na kutangaza vita vya kusambaza virusi hivyo kwa wengine. Dorothy anawashauri wajilinde wenywe. Anatahadharisha  kuwa wanaweza kudhoofisha afya yao zaidi kwa kupata maambukizo mengine ya zinaa na kukaribisha mauti kabla ya wakati wao.

Anasema mtu akiwa muathirika hakuna njia ya kubadili hali yake kuwa si muathirika, na kwamba kilicho bora kufanya ni kutafuta msaada kuweza kuishi maisha marefu kwa kutumia madwa na kula vizuri. Dorothy ambaye amekuwa mwenyekiti wa chama cha wanawake wanaosihi na ukimwi nchini Kenya kinachojulikana kwa kifupi kama WOFAK, anawapa matumaini waathiriwa wa HIV na Ukimwi na anaandika kitabu kuhusu maisha yake na wanawake wengine walioathiriwa lakini wanaoishi maisha ya kawaida.
Na kwa hakika ikiwa wewe ni muathiriwa au una mtu aliyeathirika na virusi vya HIV na Ukimwi fahamu kwamba yapo  matumaini na mifano dunia hii na haswa Afrika ni chungu nzima. Ishi kwa matumaini.

0 comments:

Chapisha Maoni

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595