Jumamosi, 28 Desemba 2013

WATU 364 WANASUBIRI ADHABU YA KUNYONGWA TANZANIA

Wadhifa wa Urais wa Tanzania umeendelea kujikuta njia panda kila unapofika wakati wa kuidhinisha kutekelezwa kwa adhabu ya kifo kwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na mahakama, na suala hilo limekuwa gumu kutekelezwa katika awamu zote nne za uongozi.
Hukumu hiyo ni kama haitekelezeki na pengine mafaili yaliyobeba uamuzi wa mahakama wenye adhabu za vifo, yameendelea kusubiri kusainiwa tangu enzi za uongozi wa awamu ya kwanza wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na hata sasa Rais Jakaya Kikwete.
Watangulizi wengine wa Rais Kikwete ni Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Pili na Mzee Benjamin Mkapa, aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Tatu. Wote wanatajwa kwamba walikuwa wazito kuidhinisha utekelezaji wa hukumu hiyo ya kuondoa uhai wa mtu.
Inaaminika kuwa Serikali za awamu ya kwanza na ya pili zilitekeleza kwa sehemu hukumu hizo, lakini Serikali zilizofuata hazikuwahi kufanya hivyo. Hii inamaanisha kuwa hakuna mtu aliyewahi kunyongwa kwa miaka 18 iliyopita.
Takwimu zilizotolewa na Jeshi la Magereza kwa gazeti hili zinaonyesha kuwa, hadi Oktoba 15, 2013 kulikuwa na watu 364 katika magereza mbalimbali nchini wanaosubiri kunyongwa, baada ya kuhukumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania. Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamishna wa Magezera (CP), Dk Juma  Malewa iliweka bayana kuwa hadi wakati huo, wafungwa 86 walikuwa wamekata rufani za kupinga hukumu katika Mahakama ya Rufani Tanzania.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema anasema hawezi kufahamu kwanini Marais wameshindwa kusaini hukumu za vifo kwa muda mrefu, kwani suala hilo lina michakato na mambo mengi ndani yake.
Hata hivyo anaongeza kuwa kutokana na Tanzania kufuata utaratibu wa maadili (moral) katika utawala wake, inaweza kuwa chanzo cha ugumu wa utekelezaji wake.
Hukumu ya Kifo hutolewa chini ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act. 1985) ambayo inasisitiza kuwa utekelezaji wa hukumu hiyo ni muhukumiwa kunyongwa na siyo vinginevyo.
Kifungu cha 322 cha sheria hiyo kinasema endapo mtu atahukumiwa kwa sheria hiyo, atalazimika kunyongwa mpaka kufa.
Utata wa kusaini
Akifafanua utaratibu wa kufikia hatua ya mwisho katika utekelezaji wa hukumu hiyo, Jaji Werema anasema kabla ya rais kusaini, hukumu hiyo hupitia Mahakama Kuu na ile ya Rufani.

“Ikitoka Mahakama Kuu inapelekwa rufaa ndiyo inapitishwa ili kujithibitishia na kuondoa utata wote unaoweza kuleta matatizo ya hukumu hiyo, ni lazima kujihakikishia vya kutosha maana mtu akishanyogwa kwa bahati mbaya huwezi kurejesha uhai wake,” anasema Werema.
Alisema kabla ya rais kusaini katika hatua ya mwisho ni lazima Rais akutane na kamati ya huruma inayomshauri juu ya  kusaini hukumu hiyo. “Kitakachoshauriwa na kamati hiyo kwa Rais, ndiyo ataamua kusaini ama kutosaini, huwa kuna mambo mengi yanayoangaliwa,” alisema.
Wakati kukiwa na utata wa kusaini hukumu za kifo, Mtaalamu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo anasema mtu anayesubiria hukumu ya kunyongwa ni sawa na mtu aliyekufa kiakili.
Anasema kinachobakia ni maumbile ya mwili na roho tu visivyokuwa na msaada wowote kwake katika mazingira hayo.  “Huishi kipindi kigumu sana kuliko mwanadamu yeyote yule anayeishi hapa duniani, utashi, hisia na kufikiri kwake hakufanyi kazi,” anasema Dk Ktila.
Dk Kitila anasema kisaikolojia hukumu hiyo imegundulika kuwa na madhara makubwa kuliko zote duniani, kwani inaweza kumuathiri kwa muda mrefu hata kama atabahatika kupata msamaha wa kutohukumiwa hukumu hiyo.
Dk Kitila anasema endapo atasamehewa hukumu hiyo na kurudi  kwenye jamii, atalazimika kuwa chini ya uangalizi kwa kipindi kirefu mpaka atakaporudia hali yake kama binadamu wa kawaida.
“Anakuwa kama amezaliwa upya, ni vigumu ubongo kurudia hali yake kwa haraka hivyo ili kuepusha madhara ya kuchanganyikiwa akili, kichaa au vinginevyo ni lazima apate mtu wa kuishi naye,” anasema.
Anabainisha kuwa kwa mujibu wa matokeo ya kisaikolojia, asilimia kubwa wanawake ndiyo huathirika zaidi kuliko wanaume.
Msimamo wa Tanzania
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikishinikizwa na mashirika ya kimataifa hasa yale ya utetezi wa haki za binadamu kufuta sheria hiyo.
Machi 6 mwaka huu Kamishna wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay alinukuliwa kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akilaani kuendelea kwa adhabu hiyo alioyoiita kuwa ni “ukatili dhidi ya binadamu”.
Hata hivyo Jaji Werema anasema hukumu ya kifo itaendelea kutolewa mpaka pale sheria husika itakapofanyiwa marekebisho na kwamba Serikali inalazimika kuendelea na adhabu hiyo kutokana na matukio ya kinyama yanayoendelea katika jamii.
“Sheria ya hukumu hiyo bado ipo katika vitabu vya Serikali hivyo mahakama itaendelea na utekelezaji wake, hata wananchi ukiwaambia wapige kura kuifuta hawatakubali kwa sasa kutokana na mauaji ya albino,” anasema Jaji Werema.
Werema anaungwa mkono na Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha na utetezi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ‘Under the Same Sun’, Vicky Ntetema ambaye anasisitiza kwamba  utekelezaji wa hukumu hiyo ni muhimu hususani kwa wauaji wa albino ili kukomesha ukatili huo.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe akizungumza kupitia mahojiano ya kipindi cha dakika 45 cha Kituo cha Televisheni cha ITV alisema “hukumu hiyo ni mbaya na haipaswi kuendelea kwa sasa”.
Chikawe anasema tangu adhabu hiyo imeanza kutumika, haijaonyesha mafanikio yoyote ya kupunguza matukio ya uharifu nchini.
“Imepitwa na wakati na ndiyo maana hata nchi nyingine zimeshaiacha, binafsi nisingependa tuendelee kuwa nayo na badala yake tuwe na mbadala wa hukumu kifungo cha jela pekee,” alisema.
Kauli ya Chikawe inaungwa mkono na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu  (LHRC), ambacho pia kinapinga adhabu hiyo na kusisitiza kufutwa kwa sheria husika.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba anasema adhabu hiyo inatakiwa kupigwa vita hapa nchini na duniani kote kwani imepitwa na wakati na kwamba ni adhabu inayoharibu taswira ya nchi na kulifanya taifa lionekane kama eneo la wahalifu wa mauaji (degrading). “Lakini pia hukumu hiyo ni vigumu kuthibitisha ukweli wa uhalifu uliotendwa na wahukumiwa hao na ikitolewa kwa makosa huwezi kurudisha uhai wa mtu aliyenyongwa kwani kumekuwapo na ushahidi huo,”anasema Dk. Bisimba.
Anaongeza kuwa adhabu hiyo mpaka sasa haina ushahidi wowote wa kuzuia watu wengine kutenda makosa husika.
Ripoti ya Dunia
Aprili 10, mwaka huu shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International linalopinga adhabu hiyo lilitoa ripoti juu ya hukumu hiyo likisema mwaka 2012 kuna baadhi ya nchi duniani ziliendelea na ukutekelezaji wa hukumu hiyo.
Katika mataifa mbalimbali duniani, hukumu hiyo imekuwa ikipungua na nyingine zikiifuta.
Shirika hilo limeripoti kuwa mwaka jana nchini Iran takribani watu 314 walinyongwa, wengine 79 nchini Saudi Arabia huku Marekani ikitekeleza hukumu hiyo kwa majimbo kadhaa ikiwanyonga watu 43, idadi sawa na mwaka 2011.

0 comments:

Chapisha Maoni

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595