Jumanne, 19 Agosti 2014

Albino wazua tafrani Polisi Bugurun


Dar es Salaam. Watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), jana walizua tafrani Kituo cha Polisi Buguruni, wakipinga dhamana kwa mshtakiwa, Ombeni Swai (34), mkazi wa Tabata Matumbi anayekabiliwa na kesi ya kutoa vitisho vya kumuua mwenzao.
Tafrani hiyo ilianzia katika Mahakama ya Mwanzo Buguruni baada ya mshtakiwa huyo kusomewa mashtaka na Karani wa Mahakama, Edwin Wandanda na kisha Hakimu Mfawidhi, Benjamin Mwakasonda aliyekuwa akiisikiliza kusema dhamana ya mshtakiwa iko wazi.
Ingawa mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana, albino waliokuwapo mahakamani hapo hawakufurahishwa na kitendo cha kuwapo kwa nafasi ya dhamana kwa mshtakiwa wakidai kwamba ameshatoa vitisho vya mauaji dhidi yao.
Baada ya kulalamika mahakamani hapo waliandamana hadi kituoni hapo ambako mshtakiwa alikuwa amepelekwa hali iliyosababisha polisi kituoni hapo kutumia risasi za baridi kuwatawanya na kusababisha taharuki kwa wafanyabiashara na wakazi wa eneo hilo.
Mwandishi wetu alishuhudia baadhi ya watu wakiwa wamesimama, wengine wakikimbia ovyo huku polisi wakiwa silaha.
Kamanda wa Mkoa wa Polisi Ilala, Mariam Nzuki alisema vurugu hizo ziliongezeka baada ya kundi la vijana wa sokoni kuungana nao.
Alisema baada ya polisi kuona hivyo, walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya na kumpeleka mtuhumiwa katika Mahabusu ya Segerea.
Hati ya mashtaka
Mshtakiwa anadaiwa kuwa Agosti 16, mwaka huu maeneo ya Buguruni kwa Mkanda alitishia kuua kwa maneno watu wenye ulemavu wa ngozi katika maeneo hayo.
Hati hiyo inadai kuwa mshtakiwa alimtishia kwa maneno mlalamikaji, Mwinyiusi Issa kuwa atamuua kama anavyoua albino.
Mengi ajitolea
1 | 2 Next Page»

PAPA AMEKUBALI PADRI MOSHA KUOA


Moshi. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amekubali kumuondolea sakramenti ya upadri, Raymond Mosha wa Jimbo Katoliki la Moshi ikiwa ni miaka 20 tangu padri huyo aombe kuachana na daraja hilo.
Barua ya uamuzi wa Papa Francis ilisomwa juzi katika parokia na vigango vyote vya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi katika ibada zilizofanyika katika makanisa ya jimbo hilo.
Miongoni mwa parokia ambazo barua hiyo ilisomwa ni Karanga ambako Paroko wake, John Matumaini alitoa tangazo hilo katika ibada zote. Uamuzi huo ambao ni nadra kutolewa na Papa, unamaanisha kuwa sasa padri huyo yuko huru kuoa na kuwa na familia.
Hata hivyo, wakati uamuzi huo ukitangazwa rasmi juzi, tayari Padri Mosha ambaye ni profesa wa falsafa na maadili katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela Arusha, ana mke na watoto watatu ambao kwa sasa wako vyuo vikuu.
Padri Mosha alisema aliandika barua kuomba kuondolewa daraja hilo mwaka 1994 kabla ya uamuzi kutolewa juzi.
Katika orodha ya mapadre 185 wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi iliyopo katika tovuti ya jimbo hilo, jina la Padri Mosha linaonekana likiwa ni namba 23.
Akizungumzia hatua hiyo, Padri Mosha alisema: “Ninafurahi kufunguliwa kifugo hiki na hii itanifanya niishi kama Mkristo. Kwa vile hawajaniondolea sifa ya kutoa huduma kama vile ibada za mazishi, sakramenti ya mwisho na ubatizo, nitaendelea kutoa kwa wahitaji kwa sababu ninaupenda ukristo.
“Nashukuru sasa nimekuwa muumini wa kawaida nitaweza kufunga ndoa kanisani kwa kuwa nilikuwa nimefunga ndoa ya kisheria tu kwa DC.”
Kuhusu kwa nini aliamua kuacha upadri, Profesa Mosha alisema ni baada ya kufanya kazi hiyo kwa miaka 20 na akaona ipo haja ya kuwa na familia lakini kanisa lilikuwa haliruhusu.
“Sasa kwa kuwa kanisa haliruhusu mapadri kuoa ndiyo maana nikaamua kuandika barua ambayo hata hivyo, imechukua muda mrefu kujibiwa na tayari nina watoto watatu wako chuo kikuu.

Jaji Lewis Makame afariki dunia


Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 chini ya mfumo wa vyama vingi, Jaji Lewis Makame amefariki dunia.
Taarifa iliyopatikana jana jioni na kuthibitishwa na mwanaye, Eugene Makame, Jaji Makame alifariki dunia jana mchana katika Hospitali ya AMI Trauma, Masaki Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa takribani mwezi mmoja.
“Nasikitika kuwataarifu ya kwamba mzee (Jaji Makame) hatunaye tena, Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe mbele yake, nyuma yetu, Amen,” alisema Eugene kupitia ujumbe mfupi wa maneno akieleza kuhusu kifo hicho.
Jaji Makame alilazwa katika hospitali hiyo tangu mwishoni mwa Julai, mwaka huu lakini hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu kuugua kwake na maradhi yaliyokuwa yakimkabili.
Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Rais Jakaya Kikwete walimtembelea hospitalini hapo. Wengine ni Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan, Jaji Joseph Warioba na Mwenyekiti wa sasa wa NEC, Jaji Damian Lubuva.
Wasifu wake
Jaji Makame aliiongoza NEC tangu mwaka 1993 hadi mkataba wake wa utumishi wa umma ulipofikia ukomo, Julai mwaka 2011.
Aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Januari 14, 1993 kushika wadhifa huo na alisimamia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini, ambao Benjamin Mkapa (CCM) aliwashinda wapinzani wake, Augustine Mrema (TLP) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF).
Pia, ndiye aliyesimamia uchaguzi ambao ulimwingiza madarakani Rais Kikwete mwaka 2005 na 2010.
Kabla ya kuteuliwa kwake kuingia NEC, Jaji Makame alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Miongoni mwa makamishna saba wa kwanza wa NEC waliofanya kazi naye ni Jaji Augustino Ramadhan, ambaye pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC, aliyetokea pia Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Jaji Mark Bomani, Solomon Liani, Ben Lobulu, Jaji Julie Manning na Masauni Yussuf Masauni.
Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume za Uchaguzi kwa Nchi Wanachama wa Ushirikiano Kusini mwa Afrika (SADC), Mjumbe wa Taasisi ya Demokrasia Endelevu Afrika, (EISA). Kitaaluma, alisoma Shahada ya Sayansi Jamii katika Chuo Kikuu cha London, Uingereza kisha masomo ya sheria nchini humo alikohitimu kozi ya Barrister-At Law, mwaka 1964.

Alhamisi, 2 Januari 2014

DUNIA YAUPOKEA MWAKA 2014 KWA SHANGWE

Dunia imeukaribisha mwaka mpya wa 2014 kwa fataki, chereko, shangwe kubwa na kutakiana kheri. Sherehe kubwa zilizofanyika Dubai na mji mkuu wa Ujerumani, Berlin ni mfano wa zile zilizotia fora

 Dubai imevunja rekodi ya dunia kwa maonyesho makubwa kabisa ya fataki kuwahi kushuhudiwa katika Mkesha wa Mwaka Mpya yaliyohusisha fashifashi nusu milioni.
Fataki hizo zilin'gara angani kwa dakika sita na kutanda kwenye mwambao wa Dubai wa kilomita 100, kivutio kikuu cha fataki hizo kikikiwa kutoka kwenye jumba refu kabisa duniani la Burj Khalifa lenye urefu wa mita 830 na katika hoteli ya kifahari ya Atlantis ilioko Palm Jumeira, mojawapo ya visiwa vitatu vilivyotengenezwa na binaadamu kikiwa na umbo la mtende.
Rikodi ya mwisho iliwekwa na Kuwait hapo mwaka 2011 kwa onyesho la fataki 77,282 lililodumu kwa saa nzima.
Wananchi wa Ujerumani wameukaribisha mwaka mpya kwa onyesho kubwa la fataki na vifijo ambapo tafrija kubwa kabisa ililifanyika mjini Berlin katika Lango la Brandenburg ambapo mamia kwa maelfu walihesabu kwa pamoja dakika za lala salama kabla ya kuingia mwaka mpya.
Milango ya kuingia kwenye eneo la tafrija hiyo ilibidi kufungwa na mapema kutokana na umma mkubwa uliofurika kuhudhuria tafrija hiyo ambapo inakadiriwa kwamba watu milioni mbili walimiminika mjini humo kwa ajili ya sherehe hiyo ya kuaga mwaka na kukurabisha mwaka mpya. Mjini London ambapo mwaka mpya umeingia saa moja baada ya kupokelewa nchini Ujerumani takriban watu 50,000 waliushangilia kwa maonyesho ya fataki kwenye kingo za Mto Thames wakati kengele ya saa kuu ilioko kwenye la jengo la bunge la nchi hiyo mjini London ikihanikiza ilipotimia sita za usiku kuashiria kuingia kwa mwaka mpya.
Nchini Urusi maelfu ya watu wameukaribisha mwaka mpya kwa onyesho la fataki katika uwanja wa "Red Square" mjini Moscow lakini kwa desturi kutokana na kupishana kwa wakati katika majimbo mengi ya Urusi watu hawaukaribishi mwaka huu kwa wakati mmoja na kengele ya kuingia kwa mwaka mpya hulia kwenye saa ya Mnara wa Ikulu ya Kremlin tarehe 1 Januari.
Kutokana na mashambulizi ya kigaidi katika mji wa Volgograd miji mingi nchini Urusi imeimarisha usalama au kufuta kabisa sherehe za mwaka mpya.
Watu wanaofikia milioni mbili na laki tatu wamejimwaga katika pwani mashuhuri ya Copacabana mjini Rio de Janeiro nchini Brazil kuukaribisha mwaka mpya kwa maonyesho ya tani 24 za fataki na muziki wakati nchi hiyo mwaka huu ikiwa mwenyeji wa michuano ya soka kuwania Kombe la Dunia.
Visiwa vya Kiribati na Samoa huko Pasifiki vilikuwa vya kwanza kuushuhudia mwaka mpya duniani ikifuatiwa na New Zealand kabla ya watu milioni 1.6 katika bandari ya Sydney nchini Australia ambao ni mji mkubwa kabisa nchini humo kuukaribisha mwaka huo kama kawaida kwa onyesho la shani la tani saba za fataki katika fukwe za Jengo la Opera.
Hawakujali baridi

Mjini New York watu wanaokadiriwa kufikia milioni moja wakivumilia baridi kali na baadhi yao wakiwa wamepiga kambi tokea asubuhi kwa ajili ya kujipatia nafasi nzuri ya kujionea shamra shamra za kuukaribisha mwaka mpya walihesabu kwa sauti moja dakika za mwisho kuingia mwaka mpya.

Vipaza sauti vilihanikiza kwa wimbo wa kitambulisho wa Frank Sinatra "New York, New York" katika dakika za kwanza za kuanza kwa mwaka mpya na wanaanga watatu wa anga za juu kutoka Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu walijitokeza kwenye kioo kikubwa cha Televisheni kuutakia umati uliofurika hapo heri ya mwaka mpya.
Visiwa vya mbali vya Marekani vya Howland na Baker vitakuwa vya mwisho kuukaribisha mwaka mpya.
Asia yazingatia mila
Nchini Japani mamilioni ya watu wamezuru mahekalu kuukaribisha mwaka mpya kwa tafakuri na kuombeana dua.
Mjini Seoul Korea Kusini kengele ya shaba ya karne ya 15 imepigwa mara 33 kwa kuzingatia mila ya kale ya mwaka mpya.
Nchini Indonesia ngome kuu ya Sharia ya Kiislamu Banda Aceh sherehe za mwaka mpya zimepigwa marufuku kwa mara ya kwanza huku polisi wa itikadi kali za Kiislamu wakitaifisha maelfu ya fataki na matarumbeta yaliokuwa yatumike kuukaribisha mwaka.

Afrika ya Kusini nayo imeuaga mwaka 2013 kwa video ya kumuaga hayati Nelson Mandela wakati nchi hiyo ikianza mwaka mpya bila ya kuwa na shujaa wao huyo kipenzi.
Sura ya Mandela, rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo, imetanda kwenye ukumbi wa jiji wa Cape Town ambapo hapo mwaka 1990 alitowa hotuba yake ya kwanza baada ya kuwa kifungoni kwa miaka 27 chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

HALI YA AFYA YA ARIEL SHARON INAZIDI KUZOROTA

Hali ya kiafya ya waziri mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon - ambaye amekuwa katika hali mahututi, inaendelea kuzorota zaidi.
Inaarifiwa kwamba maisha yake yamo hatarini.
Madaktari wanasema kuwa Sharon mwenye umri wa miaka , 85, anakabiliwa na matatizo ya afya ya viongo vyake vya mwili ikiwemo Figo zake na kwamba vinaanza kuonekana kutofanya kazi vyema.
Hata hivyo madaktari hawakutoa taarifa zaidi kuhusu afya ya Sharon.
Alichukua wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2001 na kuugua kiharusi mwaka 2005 na alisifika sana kwa msimamo wake mkali kuhusu hali ya kisiasa kati ya taifa hilo na utawala wa Palestina.
Baada ya kupatwa na kiharusi kingine mwaka 2006, Sharon akapotewa na fahamu na amekuwa kwenye mashine ya kusaidia moyo wake kuendelea kupiga tangu hapo.
Sharon alikuwa mmoja wa wanasiasa mashuhuri wenye utata katika siasa za Israel.

MAPIGANO MAKALI YANAENDELEA SUDANI KUSINI

Mapigano yanaendelea nchini Sudan Kusini licha ya pande mbili zinazohusishwa na mgogoro wa nchi hiyo kujiandaa kwa mazungumzo ya amani nchini Ethiopia.
Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini ameiambia BBC kuwa mapigano yanaendelea katika mji wa Bor na baadhi ya sehemu za jimbo la Unity.
Pande zote mbili za serikali na waasi wamepeleka wajumbe wao katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Mpaka sasa waasi wamekataa kusitisha mapigano, wakati mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mgogoro huo yakiendelea.
Mashirika ya misaada yamesema msaada wa dharura unahitajika haraka kwa maelfu ya watu waliolazimika kuyakimbia makaazi yao.
Hali imezidi kuwa mbaya katika kambi ya wakimbizi ya Awerial iliyopo katika kingo za mto Nile- ambako sasa ni makaazi ya watu 75,000 waliokimbia mapigano jirani na Bor, mji mkuu wa jimbo la Jonglei, ambalo kwa sasa linadhibitiwa na waasi. Mji wa Bor umekuwa ukibadilishwa udhibiti wake kati ya majeshi ya serikali na waasi, kutokana na umuhimu wake. Mara ya kwanza ulitwaliwa na waasi, lakini ukakombolewa na majeshi ya serikali na sasa umerudi tena mikononi mwa waasi.
"Hakuna maji safi ya kunywa. Visima vitano- havitoshi," David Nash wa shirika la madaktari wa MSF ameiambia BBC.
"watu wanakunywa maji moja kwa moja kutoka mto Nile. Yna matope, si mazuri. Na hakuna vyoo, kwa hiyo magonjwa ya kuambukiza yanajitokeza. Kutokea kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, ni hali inayowezekana kabisa kutokea.

JESHI LA POLISI LAPATA IGP MPYA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimwapisha Inspekta Generali wa Polisi (IGP) mpya Afande Ernest Mangu katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam.

Singida. Mama Mzazi wa Mkuu wa  Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, Mwanaidi Msengi, amemsihi mwanawe kufanya kazi kwa bidii asimwangushe Rais Jakaya Kikwete ili asije kujutia kumpa nafasi hiyo.
Mwanaidi alisema licha ya furaha kubwa aliyonayo,  anamuasa mtoto wake kuchapa kazi kwa bidii kama njia mojawapo ya shukurani kwa Rais Kikwete kwa kumteua akiwa mwenyeji  wa kwanza kutoka Mkoa wa Singida kushika wadhifa huo nyeti.
“Hii ni heshima kubwa sana kwangu binafsi, ndugu zake, wakazi wa Kijiji cha Kihunadi na Mkoa wa Singida, kwa hiyo lengo langu ni kumwombea mtoto wangu Mangu asimwangushe Rais... Eee Baba (Mungu) msaidie mwanangu atimize wajibu wake ipasavyo ili Rais Kikwete siku moja aseme hakukosea kumpa Mangu ukuu wa polisi,” alisema Mwanaidi.
Juzi ndugu, jamaa na marafiki walifanya hafla ndogo iliyoambatana na vifijo, nderemo na bashasha na wakazi wa Kijiji cha Kihunadi, Tarafa ya Ilongero, mkoani Singida, alikozaliwa IGP huyo huku wakidai sasa kijiji chao kitajulikana haraka ndani na nje ya Tanzania.
Walisema licha ya kujulikana, changamoto mbalimbali zinazokikabili kijiji hicho zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu mapema iwezekanavyo.
Mwanaidi alisema Mangu alianza kumwonyesha mafanikio tangu Shule ya Msingi Kinyagigi, kwani alikuwa na bidii ya kujisomea mara kwa mara alishika nafasi ya kwanza au  ya pili.
Kwa mujibu wa Mwanaidi, IGP Mangu ni mtoto wa pili kati ya saba aliowazaa.
 “Mangu ni wa pili kati ya watoto wangu saba baada ya kuolewa na baba yao, Jumbe Omari Mangu aliyefariki Aprili 27, 1988.  Jina la Jumbe linatokana na kupewa kazi ya ujumbe wa wakoloni wakati wa ujana wake,” alisema.
Wenyeji wa kijiji hicho, walisema  wamekuwa wakiamini Mangu atafika mbali kwa kushika nafasi za juu za uongozi, kutokana na uadilifu, uchapaji kazi, ukaribu wake na wananchi, uaminifu na uwazi.
Mwanaidi alisema Mangu alipofaulu kwenda sekondari alilazimika kuomba ng’ombe kwa mke mweza, ili akamuuze apate fedha za kugharimia masomo ya mtoto wake.
“Mke mwenzangu alimtoa ng’ombe wake, lakini  Mangu alipomuuza kwenye mnada pale Singida mjini, aliibiwa fedha zote na alirudi nyumbani akilia sana,” alisema.
Alisema baada ya hapo alimwambia mtoto wake kwamba, ataanza kutengeneza vyungu kwa kutumia udongo wa mfinyanzi  ili kupata fedha za kugharimia masomo yake. “Nashukuru Mangu alinielewa vizuri kwa sababu alishiriki kubeba kichwani vyungu hivyo wakati wa kuviuza hadi kichwa chake kilikaribia kuwa kipara.  Nilibuni chanzo kingine cha mapato ambacho kilikuwa ni kukoroga na kuuza pombe za kienyeji,” alisema. Inadaiwa baba yake, IGP  Mangu alioa wanawake sita kwa nyakati tofauti, lengo likiwa ni kupata mtoto wa kiume.  Wengi wa wake zake walikuwa wakizaa watoto wa kike

Jumamosi, 28 Desemba 2013

WATU 364 WANASUBIRI ADHABU YA KUNYONGWA TANZANIA

Wadhifa wa Urais wa Tanzania umeendelea kujikuta njia panda kila unapofika wakati wa kuidhinisha kutekelezwa kwa adhabu ya kifo kwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na mahakama, na suala hilo limekuwa gumu kutekelezwa katika awamu zote nne za uongozi.
Hukumu hiyo ni kama haitekelezeki na pengine mafaili yaliyobeba uamuzi wa mahakama wenye adhabu za vifo, yameendelea kusubiri kusainiwa tangu enzi za uongozi wa awamu ya kwanza wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na hata sasa Rais Jakaya Kikwete.
Watangulizi wengine wa Rais Kikwete ni Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Pili na Mzee Benjamin Mkapa, aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Tatu. Wote wanatajwa kwamba walikuwa wazito kuidhinisha utekelezaji wa hukumu hiyo ya kuondoa uhai wa mtu.
Inaaminika kuwa Serikali za awamu ya kwanza na ya pili zilitekeleza kwa sehemu hukumu hizo, lakini Serikali zilizofuata hazikuwahi kufanya hivyo. Hii inamaanisha kuwa hakuna mtu aliyewahi kunyongwa kwa miaka 18 iliyopita.
Takwimu zilizotolewa na Jeshi la Magereza kwa gazeti hili zinaonyesha kuwa, hadi Oktoba 15, 2013 kulikuwa na watu 364 katika magereza mbalimbali nchini wanaosubiri kunyongwa, baada ya kuhukumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania. Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamishna wa Magezera (CP), Dk Juma  Malewa iliweka bayana kuwa hadi wakati huo, wafungwa 86 walikuwa wamekata rufani za kupinga hukumu katika Mahakama ya Rufani Tanzania.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema anasema hawezi kufahamu kwanini Marais wameshindwa kusaini hukumu za vifo kwa muda mrefu, kwani suala hilo lina michakato na mambo mengi ndani yake.
Hata hivyo anaongeza kuwa kutokana na Tanzania kufuata utaratibu wa maadili (moral) katika utawala wake, inaweza kuwa chanzo cha ugumu wa utekelezaji wake.
Hukumu ya Kifo hutolewa chini ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act. 1985) ambayo inasisitiza kuwa utekelezaji wa hukumu hiyo ni muhukumiwa kunyongwa na siyo vinginevyo.
Kifungu cha 322 cha sheria hiyo kinasema endapo mtu atahukumiwa kwa sheria hiyo, atalazimika kunyongwa mpaka kufa.
Utata wa kusaini
Akifafanua utaratibu wa kufikia hatua ya mwisho katika utekelezaji wa hukumu hiyo, Jaji Werema anasema kabla ya rais kusaini, hukumu hiyo hupitia Mahakama Kuu na ile ya Rufani.

“Ikitoka Mahakama Kuu inapelekwa rufaa ndiyo inapitishwa ili kujithibitishia na kuondoa utata wote unaoweza kuleta matatizo ya hukumu hiyo, ni lazima kujihakikishia vya kutosha maana mtu akishanyogwa kwa bahati mbaya huwezi kurejesha uhai wake,” anasema Werema.
Alisema kabla ya rais kusaini katika hatua ya mwisho ni lazima Rais akutane na kamati ya huruma inayomshauri juu ya  kusaini hukumu hiyo. “Kitakachoshauriwa na kamati hiyo kwa Rais, ndiyo ataamua kusaini ama kutosaini, huwa kuna mambo mengi yanayoangaliwa,” alisema.
Wakati kukiwa na utata wa kusaini hukumu za kifo, Mtaalamu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo anasema mtu anayesubiria hukumu ya kunyongwa ni sawa na mtu aliyekufa kiakili.
Anasema kinachobakia ni maumbile ya mwili na roho tu visivyokuwa na msaada wowote kwake katika mazingira hayo.  “Huishi kipindi kigumu sana kuliko mwanadamu yeyote yule anayeishi hapa duniani, utashi, hisia na kufikiri kwake hakufanyi kazi,” anasema Dk Ktila.
Dk Kitila anasema kisaikolojia hukumu hiyo imegundulika kuwa na madhara makubwa kuliko zote duniani, kwani inaweza kumuathiri kwa muda mrefu hata kama atabahatika kupata msamaha wa kutohukumiwa hukumu hiyo.
Dk Kitila anasema endapo atasamehewa hukumu hiyo na kurudi  kwenye jamii, atalazimika kuwa chini ya uangalizi kwa kipindi kirefu mpaka atakaporudia hali yake kama binadamu wa kawaida.
“Anakuwa kama amezaliwa upya, ni vigumu ubongo kurudia hali yake kwa haraka hivyo ili kuepusha madhara ya kuchanganyikiwa akili, kichaa au vinginevyo ni lazima apate mtu wa kuishi naye,” anasema.
Anabainisha kuwa kwa mujibu wa matokeo ya kisaikolojia, asilimia kubwa wanawake ndiyo huathirika zaidi kuliko wanaume.
Msimamo wa Tanzania
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikishinikizwa na mashirika ya kimataifa hasa yale ya utetezi wa haki za binadamu kufuta sheria hiyo.
Machi 6 mwaka huu Kamishna wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay alinukuliwa kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akilaani kuendelea kwa adhabu hiyo alioyoiita kuwa ni “ukatili dhidi ya binadamu”.
Hata hivyo Jaji Werema anasema hukumu ya kifo itaendelea kutolewa mpaka pale sheria husika itakapofanyiwa marekebisho na kwamba Serikali inalazimika kuendelea na adhabu hiyo kutokana na matukio ya kinyama yanayoendelea katika jamii.
“Sheria ya hukumu hiyo bado ipo katika vitabu vya Serikali hivyo mahakama itaendelea na utekelezaji wake, hata wananchi ukiwaambia wapige kura kuifuta hawatakubali kwa sasa kutokana na mauaji ya albino,” anasema Jaji Werema.
Werema anaungwa mkono na Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha na utetezi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ‘Under the Same Sun’, Vicky Ntetema ambaye anasisitiza kwamba  utekelezaji wa hukumu hiyo ni muhimu hususani kwa wauaji wa albino ili kukomesha ukatili huo.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe akizungumza kupitia mahojiano ya kipindi cha dakika 45 cha Kituo cha Televisheni cha ITV alisema “hukumu hiyo ni mbaya na haipaswi kuendelea kwa sasa”.
Chikawe anasema tangu adhabu hiyo imeanza kutumika, haijaonyesha mafanikio yoyote ya kupunguza matukio ya uharifu nchini.
“Imepitwa na wakati na ndiyo maana hata nchi nyingine zimeshaiacha, binafsi nisingependa tuendelee kuwa nayo na badala yake tuwe na mbadala wa hukumu kifungo cha jela pekee,” alisema.
Kauli ya Chikawe inaungwa mkono na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu  (LHRC), ambacho pia kinapinga adhabu hiyo na kusisitiza kufutwa kwa sheria husika.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba anasema adhabu hiyo inatakiwa kupigwa vita hapa nchini na duniani kote kwani imepitwa na wakati na kwamba ni adhabu inayoharibu taswira ya nchi na kulifanya taifa lionekane kama eneo la wahalifu wa mauaji (degrading). “Lakini pia hukumu hiyo ni vigumu kuthibitisha ukweli wa uhalifu uliotendwa na wahukumiwa hao na ikitolewa kwa makosa huwezi kurudisha uhai wa mtu aliyenyongwa kwani kumekuwapo na ushahidi huo,”anasema Dk. Bisimba.
Anaongeza kuwa adhabu hiyo mpaka sasa haina ushahidi wowote wa kuzuia watu wengine kutenda makosa husika.
Ripoti ya Dunia
Aprili 10, mwaka huu shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International linalopinga adhabu hiyo lilitoa ripoti juu ya hukumu hiyo likisema mwaka 2012 kuna baadhi ya nchi duniani ziliendelea na ukutekelezaji wa hukumu hiyo.
Katika mataifa mbalimbali duniani, hukumu hiyo imekuwa ikipungua na nyingine zikiifuta.
Shirika hilo limeripoti kuwa mwaka jana nchini Iran takribani watu 314 walinyongwa, wengine 79 nchini Saudi Arabia huku Marekani ikitekeleza hukumu hiyo kwa majimbo kadhaa ikiwanyonga watu 43, idadi sawa na mwaka 2011.

VIONGOZI WA IGAD WAJADILI MZOZO WA SUDANI

Kundi la kieneo barani Afrika linasema serikali ya Sudan  Kusini imekubali kusitisha mapigano hatua ambayo itasaidia kumalizika kwa mapigano ya makabila mbali mbali ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 mwezi huu.

Jumuiya ya nchi za pembe za Afrika- IGAD ilitangaza uamuzi huo mwishoni mwa mkutano uliofanyika ijumaa mjini Nairobi. Kundi hilo liliwasihi wafuasi wa Makamu Rais wa zamani, Riek Machar  kufanya maamuzi kama hayo.

Mapigano yalianza huko Sudan Kusini mwanzoni mwa mwezi huu baada ya Rais Kiir alipomshutumu Machar kwa jaribio la mapinduzi.

Machar anasema ghasia zilikuwa matokeo ya ulipizaji kisasi wa  mahasimu  wa kisiasa wa bwana Kiir.

Ghasia hizo haraka ziliingia katika mtazamo wa kikabila huku wafuasi wa Rais Kiir wa kundi la kabila la Dinka wakipigana na kundi la wa-Nuer ambalo anatoka bwana Machar.

Katika mkutano wa Ijumaa, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alitoa wito kwa pande zote kufikia muafaka. “Tuna fursa ndogo sana kuhakikisha amani ambapo tunawasihi wadau wote kusitisha mapigano ikiwemo Riek Machar”.

Bwana Kenyatta anasema ghasia zinaweza kutishia uthabiti wa kieneo. “Kama ghasia za hivi sasa zinaendelea na ghasia za huko zinasababisha vifo dhidi ya raia, zitasababisha  mgogoro wa kiulimwengu ambao itakuwa  vigumu zaidi kwa sudan Kusini na eneo kufikia suluhisho”.

Rais Salva Kiir
Awali Rais Kiir na Machar wote walisema walikuwa tayari kwa mashauriano lakini serikali ilikataa madai ya Machar kwamba viongozi wa upinzani waliofungwa kwanza waachiwe.

Ijumaa shirika la habari la Reuters lilisema majeshi ya serikali yaliwazidi nguvu wapiganaji wanaomtii Machar huko Malakal, mji mkuu wa jimbo la Upper Nile linalozalisha mafuta.

Alhamisi  Umoja wa Mataifa ulisema ulitarajia  kupeleka jeshi la walinda amani huko Sudan Kusini katika muda wa ndani ya saa 48.

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Hilde Johnson alielezea umuhimu wa haraka wa kuongeza jeshi la Umoja wa mataifa. Alisema zaidi ya raia 50,000 walitafuta hifadhi ya kisiasa kwenye vituo vya Umoja wa Mataifa nchini humo tangu mapigano yalipozuka.Johnson aliwasihi viongozi wa kisiasa nchini humo kuzungumza na majeshi yao na kufanya kazi pamoja ili kuleta amani. 
 

RAIS JAKAYA KIKWETE AREJEA KUTOKA MAREKANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili nchini jana, Ijumaa, Desemba 27, 2013, akitokea New York, Marekani.
Rais Kikwete amekuwa New York kwa wiki moja kwa shughuli za kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mjini Dar es Salaam, Rais Kikwete amelakiwa na viongozi mbali mbali wakiongozwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal.
 
 
Makamu wa Rais Dk.Mohamed Gharib Bilal akimlaki Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete muda mfupi baada ya Kuwasili nchini akitokea jijini New York Marekani ambapo alikwenda kwa ukaguzi wa kawaida wa afya yake.Akiwa nachini Marekani Rais Kikwete alialikwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban ki Moon nakufanya naye mazungumzo kuhusu ushiriki wa majeshi ya Tanzania katika ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali.

Makamu wa Rais Dk.Mohamed Gharib Bilal akizungumza na Rais Dkt.Jakaya Kikwete Mrisho mara baada ya kumlaki muda mfupi baada ya Kuwasili nchini akitokea jijini New York Marekani ambapo alikwenda kwa ukaguzi wa kawaida wa afya yake nchini Marekani. Rais Kikwete alialikwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki Moon na kufanya naye mazungumzo kuhusu ushiriki wa majeshi ya Tanzania katika ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali.

Ijumaa, 27 Desemba 2013

WANAJESHI NCHINI SOMALIA WAMEUAWA KWA BOMU

Takriban wanajeshi watano na afisa wa jeshi wameuawa katika mlipuko wa bomu mjini Mogadishu,nchini Somalia mashuhuda wameeleza.
Mlipuko huo unaelezwa kutokea wakati wanajeshi hao wakipata malipo yao nje kidogo ya mji huo.
Sababu ya mlipuko huo haijafahamika,majeruhi kadhaa wamepelekwa hospitalini kwa matibabu.
Wanamgambo wa kiislamu, al Shabab walitimuliwa kwa nguvu mjini Mogadishu mwaka 2011 lakini wameendelea kufanya mashambulizi nchini humo
Kundi hilo lenye uhusiano na kundi la kigaidi la al -Qaeda linadhibiti maeneo kadhaa katikati ya Somalia.

Jumatano, 18 Desemba 2013

PAPA ASHEREHEKEA MIAKA 77 YA KUZALIWA KWAKE NA WATU MASKINI

Papa Francis wa kanisa Katoliki duniani amesherehekea siku yake ya kuzaliwa kwakuwakaribisha watu wasiojiweza wanne ambao walijumuika na wageni wengine pamoja na Papa kupata kifungua kinywa alichoandaa mahususi kwa kutimiza miaka 77 tangu azaliwe, katika makazi ya Mtakatifu Martha yaliyopo Vatican nchini Italia.

Papa Francis aliwaalika watu hao pamoja na wafanyakazi wa Vatican waliojumuika na familia zao katika makazi hayo ambayo amekuwa akiishi tangu achaguliwe kuwa Papa ambayo pia yamekuwa yakikaliwa na mitume na viongozi mbalimbali wa kanisa hilo. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na radio ya Vatican imeendelea kuripoti kwamba watu hao ni kati ya kundi kubwa la watu wasio na makazi ambao hulala nje ya viunga vya Mtakatifu Peter.

Aidha katika picha zilizotolewa zimemuonyesha Papa Francis akizungumza na watu watatu kati ya wanne aliowaalika akiwemo mmoja aliyeonekana akiwa amembeba mbwa. Taarifa ya Vatican imesema tukio hilo lilikuwa lakirafiki zaidi huku waziri wa mambo ya ndani wa Vatican Pietro Parolin amemtakia heri Papa Francis katika siku yake ya kuzaliwa.
Papa akiwa na watu wasio na makazi nje ya Vatican

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595