ALI Omar, mkazi wa Kijiji cha Mabana, wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro anashikiliwa na polisi kwa kosa la kumkata miguu Said Iddi kwa kumtuhumu kumfumania na mkewe aliyejulikana kwa jina la mama Ali.
Tukio hilo la kikatili lilijiri Julai 15, mwaka huu wakati Said na mama Ali walipokuwa ndani ya nyumba ya Ali iliyopo kijijini hapo.
MANENO YA SHUHUDA
Akizungumza na mwandishi wetu, shuhuda mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja alisema Said alifumaniwa ndani ya nyumba asubuhi akiwa na mke wa Ali baada ya kuwekewa mtego ambao ulimnasa vizuri.
“Ali alipewa habari na kijana mmoja aitwaye God kwamba mkewe si mwaminifu katika ndoa, akamwongezea kuwa anatoka kimapenzi na Said. Ndipo Ali na mnyetishaji wake huyo walipopanga kumfumania jamaa,” alisema shuhuda.
Aliongeza kudai kuwa, Said ni msimamizi wa mashamba ya Ali kijijini hapo na kwamba God ni mtoto wa mwenye nyumba ambayo Ali amepanga kijijini hapo.
MPANGO WA FUMANIZI
Habari zinapasha kuwa mara baada ya mnyetishaji kutoa taarifa za usaliti huo, Ali alimtafuta ‘baunsa’ ambaye jina lake halikuweza kujulikana mara moja na wakaweka mtego kwa kujificha karibu na nyumba hiyo ambayo Said angeingia ili kuivunja amri ya sita ya Mungu.Katika kufanikisha mtego huo, mmbeya huyo alipewa jukumu la kuhakikisha nyendo za Said na mama Ali siku hiyo zinarekodiwa mpaka kuingia ndani ya nyumba hiyo na kumtaarifu Ali ambaye siku hiyo alimuaga mkewe kwamba amesafiri.
SAID ATINGA NYUMBANI KWA ALI
Habari zinasema mtoboa siri huyo alimwambia Said kuwa Ali amesafiri na ndipo jamaa akafunga safari kwenda kwa mama Ali kwa nia ya kujivinjari licha ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ukifikia katikati.
Habari zinadai mara baada ya kufika kwa Ali, Said aliingia ndani ya nyumba bila kujua kwamba mwenye mke alikuwa amejificha jirani akisubiri mtego unase.
Inasemekana Said akiwa ndani, Ali na baunsa wake waliibuka kwa kutaarifiwa na God na kumnasa jamaa huyo huku akidai ni mgoni wake. Alimuuliza maswali kadhaa, yakiwemo haya:
“Umekuja kufanya nini ndani ya nyumba yangu? Kwa nini umekaa na mke wangu?”
Habari zinasema Said alijibu hakuona ubaya kwa kuwa yeye ni mwangalizi wa mashamba ya mwanaume huyo hivyo anaweza kuingia ndani kwake wakati wowote.
Jibu hilo lilidaiwa kumtibua Ali na ndipo yeye na baunsa wake wapomfunga kamba miguuni Said na kuanza kumkata kwa panga mguu mmoja kisha kuugeukia wa pili.
Said alipiga mayowe yaliyowafanya wanakijiji kukimbilia eneo la tukio kwa lengo la kujua kulikoni ambapo walimkuta Said akiwa anavuja damu na sehemu ya nyuma ya miguu ikiwa nyanga’nyang’a.
MWENYE MKE AKIMBIA, ANASWA
Ali, God na baunsa walikimbia eneo hilo. Baadhi ya wanawake walitumia khanga zao kuifunga miguu ya Said kwa lengo la kujaribu kuzuia damu isiendelee kumwagika. Said alikuwa akilia sana.
“Wanakijiji walichukizwa sana na ukatili uliofanywa na Ali, hivyo wakaanza kumsaka na kumkamata kichakani akiwa amejificha pamoja na God. Alipewa mkong’oto kwa lengo la kutaka kumuua, lakini viongozi wa kijiji walisihi asiuawe bali afikishwe kwenye kituo cha polisi,” alisema shuhuda.
MKE, MUME, MMBEYA WAFIKISHWA POLISI
Polisi wa Kituo cha Dumila waliitwa na kumchukua Said, Ali na God kwa kutumia gari aina ya Land Rover lenye namba za usajili T 750 AAJ. Mke wa Ali yeye alipelekwa polisi kwa pikipiki.
Walipofika kituoni, Said alipewa fomu ya matibabu ya polisi (PF 3) na kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa matibabu.
“Pale hospitali Said alishonwa miguu yote lakini madaktari wakaamua ahamishiwe katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi,” alisema shuhuda huyo.
ANAWEZA ASITEMBEE TENA
Akaongeza: Daktari mmoja alisema haamini kama jamaa (Said) atatembea tena kwa sababu zana iliyotumika kumkata ilifika hadi kwenye mishipa ya nyuma ambayo ndiyo humfanya binadamu aweze kusimama na kutembea.
BAUNSA ASAKWA
Afisa mmoja wa polisi kituoni hapo ambaye hakupenda jina lake liandikwe kwa kuwa si msemaji, alisema wanaendelea kumsaka baunsa aliyeshirikiana na Ali kumkata miguu Said.
Mbaya sana!
JibuFuta