Rais Jakaya Kikwete jana alipuliza kipenga kuzindua Tamasha la
Matumaini Dar es Salaam na kuwanyooshea kidole viongozi wa dini
wanaohubiri siasa katika maeneo ya ibada akisema kufanya hivyo ni
kufilisika kifikra.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kupiga filimbi
kuashiria ufunguzi wa tamasha hilo lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema ni jambo la hatari kwa Watanzania
kukubali kugawanywa kwa misingi ya udini, rangi au maeneo wanakotoka.
Alitaka dini zitumike kuwaunganisha wananchi na
siyo kuwagawanya akisema Watanzania wanakwenda makanisani na misikitini
kusali na siyo kufanya siasa. Alisema kiongozi yeyote wa dini
anayesisitiza waumini wake kuunga mkono chama chochote cha siasa
amefilisika kifikra.
“Ni hatari tukigawanyika, ni lazima tuwaambie
watu wanaotaka kutugawanya kwa misingi ya dini, rangi au maeneo
tunakotoka kwamba hatutaki na wala hatukubali. Nchi hii wakoloni
waliishindwa hivyo lazima tuendeleze utamaduni wa kukataa kugawanywa kwa
msingi wowote ule,” alisema Rais Kikwete.
Aliwataka wanasiasa kuepuka kauli zenye kuchochea
vurugu miongoni mwa wananchi wanapokuwa kwenye harakati zao za kisiasa
akisema madaraka ya kisiasa yatafutwe kwa njia ya amani na siyo kuingiza
kauli za uchochezi zenye kuwagawa wananchi.
“Nawaasa wanasiasa wasipandikize chuki za kidini
au maeneo wanakotoka wananchi, kama ni madaraka yatafutwe kwa njia ya
amani kwenye sanduku la kura,” alisema Rais. Alisema Tamasha la
Matumaini liwe mfano wa kuigwa wa kutumia michezo kuwaunganisha watu
badala ya kuwagawanya.
Alisema timu zilizotumbuiza jana zilimebeba majina
ya Simba na Yanga, zimejumuisha wabunge kutoka vyama vyote ikionyesha
kuwa wote ni wamoja licha ya tofauti za kisiasa.
Alipongeza mkakati wa waandaaji wa tamasha hilo
ambao wametangaza kwamba mapato yatakayopatikana yatatumika kusaidia
shule za sekondari katika mikoa minane nchini.
0 comments:
Chapisha Maoni