Jumanne, 4 Juni 2013

MHE. SPIKA ASHIRIKI MAOMBEZI NCHINI UGANDA KWA AJILI YA HAYATI BABA WA TAIFA


Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Makinda (Mb), asubuhi hii ameshiriki maombezi maalumu yaliyofanyika, Namgongo nchini Uganda kwa ajili ya kumwombea Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ili atangazwe mwenye heri na hatimaye Mtakatifu sawa na imani ya dhehebu la Kikatoliki.
Maombezi haya maalumu ambayo hufanyika kila mwaka, tarehe 1 Juni mwaka huu ukiwa ni wa saba mfululizo, kuanzia mwaka 2007 katika kanisa hilo maarufu nchini humo, ambalo limejengwa mahali ambapo Mfalme wa Baganda, Kabaka Mwanga II aliamuru kuuwawa kwa Wakristo wapatao 35 kati ya miaka ya 1885 hadi 1887, walioifia imani yao na kukataa kumkana Mwokozi wao hata mauti, alimaarufu Mashahidi wa Uganda, siku ambayo huandhimishwa kila mwaka tarehe 3 Juni na kukusanya mahujaji wengi toka eneo lote la maziwa makuu, wakiwemo mamia ya Watanzania.
Mgeni Rasmi katika Ibada hiyo alikuwa Makamu wa Raisi wa Uganda, Mhe. Edward Ssekandi, akimwakilisha Rais wa nchi hiyo, Mhe. Rais Yoweri Kaguta Mseveni alisema licha ya sifa nyingi alizokuwa nazo Mwl. Kwa maisha yake ya utuetezi wa haki za wanyonge na kupigania uhuru wa Mwafrika, pia kwa uongozi wake mzuri uliompa sifa ndani na  nje ya nchi yake, Wananchi wa Uganda kamwe hawezi kumsahau kwa ajili ya vita vya Ukombozi wa nchi yao vya mwaka 1978-79.

Pamoja na Mhe. Spika, Kiongozi mwingine maarufu kutoka Tanzania aliyeshiriki maombezi hayo na kuzungumza mbele ya Waumini hao wa Kikatoliki na wengine wengi waliofurika kushuhudia tukio hilo alikua mwanasiasa mkongwe nchini, Mzee John Samwel Malecela, ambaye aliwahi pia kuwa Waziri Mkuu na Makamu Wa Pili wa Rais, chini ya uongozi wake, na kutoa ushuhuda wa jinsi Mwalimu alivyokuwa Kiongozi mnyenyekevu na asiyependa makuu, na hata kukataa kuitwa “Mtukufu Rais” kama ilivyozoeleka kwa marais wengine.
Mama Maria Nyerere na watoto wake Watatu, akiwamo mwanae  ambaye ni Mbunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki, Mhe. Charles Makongoro Nyerere, mbpia walishiriki Ibada hiyo maalumu ambayo hutangulia Siku Maarufu ya Maadhimisho ya Mashahidi wa Uganda inayofanyika Namgongo kila Mwaka. Watu wengine maarufu kushiriki Ibada hiyo alikuwa Sika wa Bunge la Afrika Mashariki, Mhe. Margaret Nantongo Zziwa, Wabunge wapatao sita kutoka Bunge hilo la Jumuiya na wengine watatu kutoka Sudani ya Kusini.
Wageni wengine maarufu waliokwishawahi kushiriki Ibada hii maalumu ya maombezi kwa ajili ya Hayati Baba wa Taifa kutoka Tanzania ni pamoja na Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mtaafu wa awamu ya tatu, aliyeshiriki mwaka 2009 na Mh. Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndg. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekwenda mwaka 2010.

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595