Jumatatu, 8 Julai 2013

MAUAJI YALIYOTOKEA CAIRO YAZIDISHA MZOZO WA KISIASA

Hali imezidi kuwa tete nchini Misri kufuatia mauaji ya waandamanaji kadhaa wanaomuunga mkono rais aliyepinduliwa Mohamad Mursi asubuhi ya leo (08.07.2013) ambayo chama cha Udugu wa Kiislamu kimesema yamefanywa na polisi.
Watu wasiopungua 42 wameuawa na wengine 300 wamejeruhiwa katika shambulio karibu na jengo la makao makuu ya kikosi cha kulinda Jamhuri, mjini Nasr ambako inaaminika rais aliepinduliwa Mohamad Mursi anashikiliwa. Chama cha Udugu wa Kiislamu kimesma yalikuwa maandamano ya amani, na walishambuliwa. Msemaji wa chama hicho, Gehad Haddad, amesema, "Wanajeshi wa kikosi cha kulinda Jamhuri pamoja na jeshi la polisi walianza kufyatua risasi za moto dhidi ya waandamanaji wakati wa sala. Tunakusanya ushahidi wa magamba ya risasi kutoka hospitali zote na tutayatoa kwa umma uone kuwa yalitokana na silaha zilizotolewa na serikali."
Msururu wa miili iliyofunikwa ulionyesha baadhi ya waliokufa, na picha nyingine zilionyesha watu waliopigwa risasi vichwani, shingoni na vifuani. Jeshi la Misri limesema kuwa kundi la watu lililowataja kama magaidi lilijaribu kuvamia jengo hilo ambamo rais aliyepinduliwa Mohammed Mursi anashikiliwa, na kwamba afisa wake mmoja ameuawa katika makabiliano hayo na wengine 40 kujeruhiwa.
Kufuatia mauaji ya leo, naibu katibu mkuu wa chama cha Al-Nour ambacho ni tawi la kisiasa la kundi la Salafi, Shabah Abdul Alim, amesema chama hicho kinajitoa mara moja katika mazungumzo ya kuunda serikali ya mpito iliyoundwa baada ya Mursi kupinduliwa. "Hii ni kama vile utawala wa zamani umerudi upya. Tumeshuhudia demokrasia ya uongo, na tukio hili litaliweka jeshi katika lawama, jambo ambalo hatukulitarajia."
Chama cha Udugu wa kiislamu chaitisha uasi wa umma
Wafuasi wa chama cha Udugu wa kiislamu wamewakamata wanajeshi wawili wa serikali na kuwatia kwenye gari kisha kuwalazimisha kutoa kauli za kumuunga mkono Mursi na kulipinga jeshi kwa kutumia kipaza sauti. Chama cha udugu wa Kiislamu kimeitisha uasi wa umma dhidi ya wale wanaotaka kutumia nguvu kuyafanya mapinduzi kuwa yao, na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kuepusha Misri kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kama ilivyo nchini Syria.

Kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Misri, Mohammed El Baradei, amesema nchi hiyo inahitaji kwa dharura maridhiano ya kitaifa na kuyalaani vikali mauaji ya leo. Wakati huo huo, Uturuki nayo imeyalaani mauaji ya Cairo ikiyataja kuwa ya kiholela. Katika ujumbe alioutuma kwenye tovuti ya twitter leo, waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, ametaka hali ya kawaida irejee Misri.
Kwa upande mwingine, thamani ya hisa katika masoko ya hisa ya Cairo imeporomoka kwa zaidi ya asilimia mbili leo asubuhi kufuatia vurugu zilizotokea. Thamani hiyo ilishuka ghafla baada ya chombo cha habari cha serikali kutangaza kuuwawa kwa watu katika machafuko ya mjini humo. Faharasa kubwa ya Misri imeshuka kwa asilimia 2.5 baada ya kuimarika kwa asilimia 7.3 Alhamisi iliyopita kufuatia taarifa za kupinduliwa kwa Mohammed Mursi.

0 comments:

Chapisha Maoni

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595