Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
(kushoto), akiwa bungeni mjini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Sengerema,William Ngeleja.
.Serikali ya Tanzania, imeagiza mitihani yote ya kidato cha nne kwa mwaka 2012, kusahihishwa upya baada ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mizengo Pinda ya kuchunguza sababu zilizosababisha matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 kuwa mabaya, kuwahi kutokea katika historia ya mitihani nchini humo.
Asilimia 60 ya watahiniwa walianguka mitihani hiyo na kusababisha serikali kuunda tume ya uchunguzi baada ya wadau wa elimu, wazazi na wanafunzi kulalamikia matokeo hayo.Tume hiyo ilichunguza sababu zilizosabisha matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 kuwa mabaya, na imependekeza kwa serikali kufuta matokeo yote ya mitihani hiyo na isahihishwe upya.
Uamuzi huo umetangazwa katika kikao cha Bunge la Tanzania linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu, William Lukuvi.
Tume hiyo, ilipewa hadidu za rejea kadhaa ikiwemo kutafuta sababu za matokeo mabaya ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012; Kubaini sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2011 hadi 2012; Kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu mara moja,kipindi cha muda mfupi, kati na kipindi cha muda mrefu. Pia Tume hiyo ilipewa jukumu la kutathmini nafasi ya Halmashauri katika kusimamia Elimu ya Sekondari katika Halmashauri zake; na kuanisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali hii ya matokeo.
Uchambuzi wa taarifa hiyo ya awali unaonyesha kuwa kutokana na uchunguzi uliofanyika, kwa muhtasari, Tume imebaini mambo muhimu kadhaa kama vile matokeo ya Kidato cha Nne kuanzia mwaka 2008 kuendelea kushuka kuliko miaka iliyotangulia kwa sababu mbalimbali ikiwemo changamoto zinazotokana na mafanikio yaliyopo sasa ya kuongezeka sana kwa Idadi ya Shule za Msingi na za Sekondari,hasa kati ya mwaka 2001 na 2013; na hivyo kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliopo Shuleni.Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 1961 hadi 2001 Idadi ya Wanafunzi wa Shule za Msingi imeongezeka kutoka Wanafunzi 486,470(1961) hadi 4,875,764 mwaka 2001, sawa na ongezeko la Wanafunzi 4,389,294
katika kipindi hicho cha takriban miaka 40.
Hata hivyo, ongezeko hilo haliendani na mazingira ya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo upungufu wa miundombinu muhimu ya shule kama vile madarasa,maabara, madawati, maktaba, nyumba za walimu, hosteli na majengo mengine muhimu ya shule. Vilevile, kuna tatizo la uhaba wa walimu,vitabu, zana za kufundishia na matatizo ya ukaguzi wa shule.
Tume imebaini pia kwamba, pamoja na Wanafunzi hawa kuwa katika mazingira yanayofanana na ya wenzao wa miaka iliyopita na kwamba ufanisi katika shule kwa ujumla umekuwa unashuka kwa sababu mbalimbali,zikiwemo za mabadiliko ya mchakato wa kuandaa na kutoa matokeo ya mtihani kwa mwaka 2012. Mfumo uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia.
Hata hivyo baadhi ya wadau wa elimu, wazazi na wanafunzi wamehoji uamuzi huo wa serikali kama hautakuwa na athari kwa wanafunzi waliofaulu na kujiandaa na masomo ya kidato cha tano na wale ambao tayari wamejiandikisha kurudia mitihani yao kwa njia ya kulipia
0 comments:
Chapisha Maoni