Alhamisi, 29 Agosti 2013

MADAWA YA KULEVYA YATAKING'OA MADARAKANI CCM

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste, Kanda ya Mbeya, William Mwamalanga ameonya kuwa, ‘kabla hata jua halijazama’ Mungu anaenda kukifuta machoni mwa uso wa dunia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na alichodai kushindwa kuwakemea wabunge wa chama hicho ambao wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
William Lukuvi
Mwamalanga, askofu ambaye amejipambanua kama mwanaharakati anayepigana vita dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya, alitoa kauli hiyo alipoombwa na mtandao wa “Fungukasasa” kutoa maoni yake juu ya kauli iliyotolewa jana Jumanne na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse.


Mchungaji Natse alimtaka Waziri Lukuvi kutaja majina ya wabunge waliotajwa kuwa wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya. Mbunge huyo alitoa hoja hiyo kufuatia maelezo ya Lukuvi kuwa, baadhi ya majina ya wabunge yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, lakini Serikali haiwezi kuwataja hadharani kwa haraka.
Lukuvi alisema: “Serikali haiwezi kutaja majina haraka kiasi hicho kwani inaogopa kukurupuka na kushindwa mahakamani, hivyo lazima tuwe makini sana na jambo hilo. Hatuwezi kukurupuka tu eti ni fulani wakati hatuna uthibitisho.
Kumbukeni wengine mpo humu ndani ya Bunge na tukianza wengi mtakwisha maana katika orodha hiyo kubwa na nanyi mmo, na orodha ni kubwa kweli ambayo wakati mwingine inatakiwa umakini wa hali ya juu.”
Akizungumzia kauli hiyo ya serikali leo Jumatano, Askofu Mwamalanga alisema: “Majibu hayo sio ya kweli. Hii ni njia ya kukwepa wajibu. Nini maana ya serikali kuwa na vyombo vya dola. Kuna namna nyingi ambazo kama serikali wanaweza kuwashughulikia wabunge na watendaji serikalini wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
Lakini hebu nikukumbushe. Hii serikali ya CCM haina nia thabiti ya kupambana na biashara ya madawa ya kulevya. Kule Mbeya kwenye kongamano la dini kuna vijana ambao waliwataja kwa majina wabunge wa CCM kuwa ndio walikuwa wakiwabebesha madawa ya kulevya kwenda kuuza, tumewakabidhi hayo majina lakini hatujasikia wabunge hao hata wakikemewa na wala CCM hakijatoa kauli hata moja juu ya hilo.
Niseme tu ukweli ninaoujua kama mtumishi wa Mungu. Ni kwamba, kwa namna mambo yanavyoenda Mungu anaenda kukifutilia mbali Chama cha Mapinduzi “kabla hata jua halijazama.”
Askofu Mwamalanga alisema kuwa, kauli iliyotolewa na Waziri Lukuvi ni sawa na lugha ya mzazi kumdanganya mtoto kuwa atamletea pipi na kumbe hamletei. Alisema: “Ni sawa na lugha ya kitoto..ile ya kumdanganya mtoto atulie ili ukamletee pipi. Inaonesha hakuna uwajibikaji. Hiyo sio lugha ya kuondoa uovu huo wa madawa ya kulevya.”
Mwamalanga ambaye aliwahi kukabidhi Ikulu orodha ya watu, wakiwemo mashuhuri, wanaotuhumiwa kufanya biashara ya madawa ya kulevya, alisema kuwa kulingana na kauli ya Lukuvi wabunge wote wanapaswa kutoka nje ya Bunge kwa kuwa tayari kauli yake inawatia doa hata wasiohusika. Alisema, vinginevyo kama serikali inataka kubaki na heshima iwashughulikie waliomo kwenye orodha ya watuhumiwa.
Askofu huyo alisema kuwa, kama serikali imeshindwa kuwashughulikia wabunge na watu wengine maarufu walioko katika orodha ya wanaotuhumiwa kufanya biashara ya madawa ya kulevya iwakabidhi watumishi wa Mungu “wawashughulikie”.
Alisema Mwamalanga:“ Kama serikali imeshindwa itupatie watu hao tutawaonesha jinsi ya kufanya na watajua kweli Mungu yupo.”
Lakini mtandao wa “Fungukasasa ulimuuliza Askofu Mwamalanga ni vipi anataka serikali imkabidhi orodha ya watuhumiwa awashughulikie ilhali yeye mwenyewe na watumishi wenzake wamekuwa wakipelekewa orodha ya watuhumiwa kisha wanaikabidhi tena serikali badala ya kushughulika nayo kiroho.”
Mwamalanga alijibu: “Ni lazima uelewe Mungu anafanyaje kazi. Sisi tuliitii mamlaka. Tulichokifanya kwanza ni kuipa nafasi yake serikali. Tumeonesha tumeitii. Sasa kama serikali imeshindwa iturudishie ili orodha hiyo tuikabidhi kwa Mungu. Ukisoma katikaZaburi 50: 15-18 unaweza kuelewa vizuri hili ninaloliongea. Unapaswa ujue kuwa hata hatua hii ambayo unaona vita inapamba moto ni matokeo ya maombi yetu.
Ni vizuri pia kufahamu kuwa, kwa maombi tunayoyafanya hatabaki mtu, hatutaki kuongozwa na waovu. Kauli kama zile za akina Lukuvi kwa kawaida huongelewa faraghani, lakini kwa maombi yetu sasa ndio maana umeona zinatolewa hadharani.”  

0 comments:

Chapisha Maoni

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595