Jumatatu, 24 Juni 2013

KATIBU MKUU WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA: TUMIENI VIPIMO SAHIHI KATIKA KILIMO

KUONDOKANA na umasikini uliopo, wadau wa kilimo wametakiwa kutafuta njia nafuu zitakazosaidia matumizi ya vipimo na viwango sahihi vitakavyowanufaisha wakulima. Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Joyce Mapunjo, wakati akifungua warsha ya matumizi sahihi ya vipimo na viwango.
Warsha hiyo iliyoandaliwa na muungano ya Asasi ya Tanzania Markets Policy Action Nodes (TM-PAN) na kufadhiliwa na Shirika la Alliance for Green Revolution in Africa (AGRA) ililenga kujadili taarifa za utafiti wa vipimo uliofanyika nchini hivi karibuni.Alisema masuala ya vipimo vinashughulikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA) na kuna umuhimu wa kuhakikisha inajumuisha wadau wengi kwa ajili ya kuleta maendeleo.Aliwataka wadau hao kujadili namna ya kuhakikisha watu wote wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu viwango hasa vile vinavyohusiana na chakula.
“Kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha kuwa viwango vinafahamika vizuri kabla hatujaingia katika gharama kubwa ya matibabu itakayotokana na matumizi yasiyo sahihi ambayo yanaweza kuepukwa,” alisema Mapunjo. Alitoa changamoto kwa wadau hao kuhakikisha wanatoa mapendekezo yanayotekelezeka, wazi na yatakayoweza kuisadia Serikali kufikia malengo ya muda mrefu.

Akitoa matokeo ya utafiti huo, mtafiti kutoka Shirika la MRA Associates, Charles Ogutu, alisema utafiti umebaini kuwa bado hakuna mfumo unaoeleweka unaodhibiti matumizi sahihi ya vipimo na viwango. Alisema miongozo mingi na kanuni imeandikwa kwa lugha isiyoeleweka kwa mkulima wa kawaida. Alisema katika utafiti huo, wamebaini kodi za mazao na masoko zinatozwa kulingana na idadi ya magunia badala ya uzito hivyo inatoa mwanya kwa wafanyabiashara kujaza lumbesa.  Alisema utafiti umeonyesha kuwa taasisi za kiserikali kama WMA, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) vina idadi ndogo ya rasilimali watu.

“Kuna baadhi ya mikoa na wilaya utakuta watumishi wawili, bila nyenzo za usafiri sasa unatarajia wataweza kufanya kazi inavyotakiwa,” alihoji Ogutu. Akichangia kuhusu utafiti huo, Mratibu wa TM-PAN, Braison Sali, aliishauri Serikali kushughulikia changamoto zote zilizoainishwa na kuongeza bajeti katika kilimo. “Ushauri wangu kwa wakulima ni kuelimishwa zaidi kuhusiana na ujanja unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kupitia lumbesa na kuanzishwa kwa mpango wa kuhifadhi vyakula katika maghala kwa kuzingatia ubora,” alisema Ogutu.

0 comments:

Chapisha Maoni

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595