BUNGE linatarajiwa kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa
2013/2014 ya Sh trilioni 18.2, baada ya wabunge kumaliza kuijadili wiki
iliyopita. Katika fedha hizo, zaidi ya Sh trilioni 10 ni za matumizi ya
kawaida na zaidi ya Sh trilioni tano ni kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo. Kabla ya kuahirisha kikao cha Bunge baada ya kipindi cha
maswali na majibu Ijumaa wiki iliyopita, Spika wa Bunge, Anne Makinda,
alisema kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Bajeti ya Serikali inatakiwa
kujadiliwa kwa siku zisizozidi saba.
“Bajeti hii imejadiliwa kwa siku nne na wabunge walioomba kuijadili
wamefanya hivyo, sasa naufunga mjadala,” alisema Spika wiki iliyopita
wakati akihitimisha mjadala huo.
Spika Makinda alisema bajeti
hiyo itapitishwa na wabunge ambao wataitwa majina mmoja mmoja na kila
mmoja kutamka ndio au hapana, kwa mujibu wa Ibara 107 (2) ya Kanuni za
Bunge.
Sehemu hiyo inasema: “Uamuzi wa Bunge wa kupitisha au
kutopitisha Bajeti ya Serikali utafanywa kwa kupiga kura ya wazi kwa
kuita jina la mbunge mmoja mmoja.”
Spika Makinda pia
aliwakumbusha wabunge kuwa Rais Jakaya Kikwete anaweza kulivunja Bunge
iwapo litakataa kupitisha Bajeti ya Serikali.
Mjadala huo wa
Bajeti ya Serikali ulifanyika kwa siku nne bila kuhusisha wabunge wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao ndiyo wanaunda Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Wabunge hao walikuwa Arusha wakati
wote wa mjadala wa bajeti ya serikali wakihudhuria mazishi ya watu
waliokufa katika mlipuko wa bomu uliotokea wiki iliyopita katika mkutano
wa uchaguzi mdogo wa udiwani huko Kata ya Soweto mkoani Arusha.
Wakati
huo huo, wabunge wa CCM jana waliketi kama Kamati ya Chama ndani ya
Bunge (Party Cuaucus), kuweka mikakati ya kuipitisha bajeti hiyo.
Habari
zilizopatikana zilisema kikao hicho kilikuwa ni cha ‘kuwekana sawa’ kwa
ajili ya kupitisha bajeti ya serikali ya mwaka ujao wa fedha leo,
ambayo imepata kutoka kwa wabunge mbalimbali wakiwamo wa chama hicho.
Wakati
wa kujadili bajeti hiyo wabunge walitoa ushauri mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kutopandishwa ushuru wa petroli na dizeli waliodai kuwa
utasababisha kupanda kwa hali ya maisha na badala yake walishauri
vitafutwe vyanzo vingine vya mapato.
Waliitaka Serikali kuacha kung’ang’ania ushuru unaotokana na bia, mafuta na sigara kila mwaka.
Mambo
mengine yaliyoshauriwa na wabunge waliochangia mjadala huo ni kufuta au
kupunguza kwa kiasi kikubwa misamaha ya kodi, haja ya serikali
kupunguza matumizi, kuboresha utendaji katika Bandari ya Dar es Salaam,
kufufua kwa ukamilifu reli ya kati, kufufua miradi ya kilimo cha
umwagiliaji maji na kuboresha kilimo, mifugo na uvuvi hasa wa bahari
kuu.
Jumatatu, 24 Juni 2013
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Call Us Now:
+255 655 732121,
+255 716 758595 / +255 762 758595
0 comments:
Chapisha Maoni