“Sikubaliani na wazo la kuanzisha Serikali tatu, huu ni mzigo kwa wananchi wa kawaida, hawa watawala wapo ambao hawatakuwa na nguvu za kiutawala.
“Wapo ambao watakosa hata amri au uwezo wa kuagiza barabara fulani ijengwe, sasa kama ni hivyo tunakwenda wapi, nawaomba Watanzania waliangalie jambo hili kwa umakini pindi muda utakapowadia,” alisema Askofu Kilaini na kuongeza:
“Kwa mawazo yangu, napenda Serikali mbili au moja, licha ya muundo wa sasa kukabiliana na changamoto nyingi.
“Naamini tukiwa na Serikali moja, ni kitu kizuri, tunaweza kusonga mbele bila matatizo yoyote kwani tumeona katika muundo wa Serikali mbili, bado watu hawakuridhika na changamoto nyingi zilizopo.
“Kumekuwa na ukakasi katika Serikali mbili, hivyo ni vema ukaondolewa kwa manufaa ya pande mbili,” alisema Askofu Kilaini.
Alisema kwamba, katika muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, unapaswa uwe mdogo na wenye kuzingatia maslahi ya wananchi.
“Kama tutafanikiwa kuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, basi tunahitaji kuwa na umakini wa hali ya juu kwenye muundo wake ambao utazingatia maslahi ya Watanzania, tusiwe na baraza la mawaziri kubwa ambalo litakuwa ni mzigo wa uendeshaji.
Kuhusu hatima ya Muungano uliopo, alisema utakuwa legelege kwa sababu utapoteza uhalisia wake.
“Ninavyoona Muungano wetu utakuwa legelege kidogo, ule uimara utapungua kwa sababu Rais atakuwa amepungukiwa na sehemu ya madaraka yake.
“Ukiangalia tunaweza kupata rais atakayekuwa anashughulikia vitu vidogo vidogo tu, sasa tangu lini ukaona duniani kiongozi wa juu anakosa madaraka ndani ya nchi yake,” alihoji Askofu Kilaini.
Alisema kama Serikali ya Tanganyika ikirudi, ni wazi itahitaji Katiba yake, jambo ambalo litaleta mgongano mwingine.