Kumekuwa na kelele za waumini nchini Ujerumani wakishinikiza askofu huyo afukuzwe kwa kukiuka taratibu.
Vatican City. Makao Makuu ya Kanisa Katoliki
Duniani (Vatican) yamemsimamisha kazi Askofu wa Jimbo la Limburg,
Ujerumani Franz-Peter Tebartz-van Elst anayekabiliwa na kashfa ya
matumizi mabaya ya fedha kwa shughuli za kifahari.
Vatican ilieleza jana kuwa uamuzi huo umechukuliwa
baada ya kuridhika kuwa Askofu van Elst amekiuka maadili yaliyowekwa na
Papa Francis kwa viongozi walioko chini yake akiwataka waishi maisha ya
uchaji, umaskini.
Hadi sasa, kumekuwa na kelele nyingi miongoni mwa waumini nchini Ujerumani wakitaka askofu huyo afukuzwe kazi.
Miongoni mwa matumizi yake makubwa ni ujenzi wa
makazi yake binafsi yaliyogharimu Euro 2.9 milioni (Dola 3.9 milioni),
ukumbi wa chakula wenye mita za mraba 63 ambao ni pamoja na mesi na bafu
yenye thamani ya Euro 15,000.
Askofu van Elst (53) amekuwa akituhumiwa kuendesha
miradi hiyo kwenye mji wa kihistoria wa Limburg, ikiwamo makumbusho,
kumbi za mikutano, kanisa dogo na nyumba ya makazi yake binafsi.
Fedha hizo zinatokana na mapato ambayo ni misamaha ya kodi kwa vikundi vya kidini nchini Ujerumani kwa mujibu wa sheria.
“Baada ya uchunguzi wa awali, Vatican imeamua
kuchukua hatua kumsimamisha na kumwondoa kwenye usimamizi wa jimbo,”
ilieleza taarifa hiyo.
“Baba Mtakatifu (Francis) amekuwa akifuatilia kwa
karibu mambo yote yanayoendelea katika Jimbo la Limbuerg,” iliongeza
taarifa hiyo.
“Hali hiyo imefikia mahali ambako kiongozi huyu hawezi kuendelea kusimamia kazi zake za kitume kama askofu wa jimbo.”
Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza ni kwa muda
gani Askofu van Elst amesimamishwa kazi, ila iliongeza kuwa itategemea
na kukamilika kwa uchunguzi, tathmini ya hali ya fedha ya jimbo na mambo
mengine.
Wiki iliyopita, Askofu van Elst alisafiri hadi
mjini Rome, Italia kwa ndege ya shirika la gharama nafuu, Ryanair
kujieleza mbele ya Papa Francis – kutokana na madai kuwa alisafiri mwaka
jana kwa ndege ya daraja la kwanza kwenda India na pia kutumia vibaya
fedha.
0 comments:
Chapisha Maoni