Shambulio la bomu lililotegwa ndani ya gari karibu na ubalozi wa
Ufaransa mjini Tripoli nchini Libya limewajeruhi watu 2 na kuzusha
hasara kubwa.Hilo ni shambulio la kwanza dhidi ya masilahi ya Ufaransa
nchini humo.
Shambulio hilo linalotajwa kuwa ni "kitendo cha kigaidi"na viongozi wa
serikali ya Libya,limejiri katika wakati ambapo hali ya usalama inazidi
kuwa mbaya,makundi ya waasi ndiyo yenye usemi na katika hali ya kimkoa
iliyogubikwa na mzozo wa Mali ambako jeshi la Ufaransa limeingilia kati
kupambana na wafuasi wa itikadi kali.Rais Francois Hollande wa Ufaransa ambae nchi yake ilishiriki katika opereshini ya kijeshi dhidi ya utawala wa Muammar Gadhafi ,amelaani shambulio hilo na kuitaka serikali ya Libya ifanye kila liwezekanalo kujua nani walikuwa nyuma ya shambulio hilo.
Duru za ubalozi wa Ufaransa mjini Tripoli zinasema walinzi wawili wa ubalozi wamejeruhiwa,mmoja wao hali yake ni mahtuti.Jengo la ubalozi wa Ufaransa limebomoka shambulio hilo lilipotokea leo asubuhi..
Tume ya pamoja ya uchunguzi imeundwa
Balozi wa Ufaransa mjini Tripoli Antoine Sivan aliyewasili mahala shambulio hilo lilikotokea,hakutaka kutoa maelezo yoyote."Tunalaani kwa nguvu kisa hiki tunachohisi ni cha kigaidi dhidi ya nchi ndugu iliyoisaidia Libya katika mapinduzi ya mwaka 2011" amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Libya Mohammed Abdel Aziz aliyefika pia mahala shambulio hilo lilikotokea leo asubuhi.Ameelezea masikitiko yake na kushadidia mshikamano pamoja na serikali na wananchi wa Ufaransa.Ametangaza kuundwa tume ya pamoja ya Ufaransa na Libya kuchunguza chanzo cha shambulio hilo.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Libya amekataa kusema chochote kuhusu sababu au nani walikuwa nyuma ya shambulio hilo.
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius anakwenda Tripoli hii leo kufuatia shambulio hilo dhidi ya ofisi yao ya Ubalozi.
Mashambulio yanaitikisa Libya tangu wimbi la mageuzi la mwaka 2011.Balozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi na watumishi watatu wengine wa ubalozi huo waliuwawa mwaka 2012.
Mara nyingi matumizi hayo ya nguvu hufungamanishwa na wafuasi wa itikadi kali,waliokuwa wakiandamwa wakati wa utawala wa Gadhafi.
0 comments:
Chapisha Maoni