Jumatatu, 22 Julai 2013

HOTUBA YA RAISI WAKATI WA KUAGA MIILI YA ASKARI WALIOUWAWA DARFUR

 
Leo ni siku ngumu sana kutakiwa kuzungumza.  Ugumu wenyewe unatokana na ule ukweli kwamba siyo siku ya furaha bali ya majonzi na huzuni kubwa kwangu, kwa taifa letu na familia za wanajeshi wetu saba marehemu ambao tumekusanyika hapa kuwaaga.  Baada ya sherehe za kutunuku Kamisheni kwa Maofisa wapya katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi, Monduli Jumamosi tarehe 13 Julai, 2013 Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange aliniarifu kutokea shambulio la kuvizia kwa baadhi ya wanajeshi wetu walioko Darfur. Kwa kuwa wakati ule mapigano yalikuwa yanaendelea, aliniambia kuwa atatoa taarifa zaidi baadae kadri taarifa zitakavyokuwa zinapatikana. 
Baadae akanipa taarifa kuwa vijana wetu 7 wamefariki na wengine 14 wamejeruhiwa.  Lazima nikiri kuwa taarifa hiyo ilinihuzunisha, kunisikitisha na kunikasirisha.  Kwa nini watu wa Darfur wawaue wanajeshi wetu ambao wamekwenda kule kuwasaidia wapate utulivu, ili kunusuru maisha yao, kuwaondolea wasiwasi na kuwawezesha wafanye shughuli zenye tija kuendesha maisha yao.  Moja kwa moja sikusita kuamini kuwa waliofanya hivyo ni watu wahalifu.
Tangu uhuru ni sera ya nchi yetu kutetea wanyonge dhidi ya ukoloni, ubaguzi, uonevu, dhuluma na watu wote walioko katika mazingira hatarishi Afrika na duniani. Njia za Kidiplomasia zilitumika na wakati mwingine JWTZ lilishirikishwa. 
Ndio maana tumeshiriki kwenye vita vya ukombozi katika nchi kadhaa zilizopo Kusini mwa Afrika. Vilevile tumeshiriki katika shughuli za kulinda amani katika nchi mbalimbali zikiwemo Liberia, Sierra Leone na Eritrea.   Hivi sasa Jeshi letu linaendelea na jukumu hilo nchini Lebanon, Cote d’Ivoire, Darfur (Sudan), Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Katika nchi zote hizo, askari wetu wanasifiwa sana kwa bidii ya kazi, uvumilivu, uhodari na nidhamu ya hali ya juu.
Wakati wote tulipoombwa na kukubali kupeleka wanajeshi wetu kutekeleza majukumu hayo, uwezekano wa wao kujeruhiwa au kufariki yanafikiriwa kutokea.  Wanakwenda kwenye maeneo yenye mapigano hivyo hatari hizo kutokea ni jambo linalowezekana.  Tahadhari zote husika huchukuliwa kuepusha hatari hizo.  Ndiyo maana hupewa mafunzo ya kutosha na silaha za kutosha.  Hata hivyo hutokea nyakati kukatokea yasiyotarajiwa kama yaliyotokea Darfur.  Pia yaliwahi kutokea Liberia.
Kufuatia tukio hilo, nilizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye alinielezea masikitiko yake makubwa kwa yaliyotokea na kutoa pole zake nyingi.  Pia alinieleza kuwa alizungumza na Rais Bashir wa Sudan akitaka wahalifu hao wasakwe, wakamatwe na kuadhibiwa ipasavyo.   Aidha, nilifanya mazungumzo na Rais Omar Al Bashir wa Sudan, ambaye naye alinielezea masikitiko yake na kutoa pole nyingi. Katika mazungumzo yangu nae nilimsisitizia umuhimu wa Serikali yake kufanya uchunguzi wa kina wa shambulizi hilo na kuwawajibisha waliohusika.  Rais Bashir alikubaliana nami na kuahidi kufanya kila linalowezekana ili ukweli ufahamike na hatua stahiki zichukuliwe. 

isi kwa upande wetu, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limeunda Bodi ya Uchunguzi inayotarajiwa kuelekea Sudan kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha shambulizi hilo.
Kwa huko Darfur, tangu shughuli za ulinzi wa amani wa UNAMID zianze mwaka 2007 walinzi wa amani 41 kutoka mataifa mbalimbali wameuawa na zaidi ya walinzi wa amani 55 wamejeruhiwa. Kwa kweli idadi hii ni kubwa mno inayohitaji kutafakariwa vizuri na wadau wote.  Pengine wakati umefika wa kuutazama upya mfumo wa kulinda amani Darfur hasa kuhusu uwezo wa kujilinda na wanajeshi wanaolinda amani.  Hapana budi uwezo wao uongezwe ili kupunguza vifo na majeruhi.  Narudia kuahidi kuwa rai hii tutaifikisha kwa mamlaka husika katika Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru serikali ya Sudan, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia tangu kutokea kwa tukio la kushambuliwa kwa askari wetu. Pia nawashukuru na kutoa pongezi kwa Waziri Shamsi Vuai Nahodha, Jenerali Davis Mwamunyange na makamanda na askari wote wa JWTZ, kwa jinsi walivyoshughulikia msiba huu tangu ilipopokelewa taarifa ya vifo vya mashujaa wetu hawa mpaka sasa.  Mmewapa heshima kubwa wanaoistahili.  Asanteni sana.
Kwa namna ya pekee, narudia kutoa pole nyingi kwa familia za wafiwa.  Nawashukuru kwa dhati kwa moyo wao wa uvumilivu na subira. Naomba mfahamu kuwa, mimi na Watanzania wote tupo pamoja nanyi katika kuomboleza vifo vya mashujaa wetu. Msiba huu ni wa taifa letu lote na watu wote wenye kupenda amani duniani.
Daima tutawakumbuka mashujaa wetu na tutaendelea kuenzi na kujivunia kazi zao na mchango wao mkubwa kwa nchi yetu na dunia kwa ujumla. Nawaomba sote tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za mashujaa wetu mahala pema peponi. Amen.
Kwa Jeshi na wanajeshi wetu wote, napenda kumalizia kwa kuwaasa kuwa yaliyotokea Darfur yasiwakatishe tamaa katika kutimiza wajibu wetu Darfur na kwingineko.  Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.  Yaliyotokea yanatukumbusha kuchukua tahadhari zaidi na kuongeza uwezo wa kujihami wa wanajeshi wetu kila wanapotumwa kutekeleza jukumu lao.
Asanteni
 
 

0 comments:

Chapisha Maoni

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595