Jumamosi, 25 Mei 2013

YULE KIJANA RAMA, MLA NYAMA YA KICHWA CHA BINADAMU AACHIWA HURU

Dar es Salaam. Mshtakiwa Ramadhan Selemani Mussa, maarufu kama ‘Rama mla vichwa’, aliyekutwa na kichwa cha mtoto kikiwa bado kinavuja damu, pamoja na mama yake Hadija Ally, wameachiwa huru.
Rama na mama yake walikuwa wakikabiliwa na shtaka moja la kumuua kwa makusudi mtoto Salome Yohana (3), kinyume cha kifungu cha 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Hata hivyo, jana Mahakama Kuu ilimwachia huru Rama baada ya kuridhika na ripoti ya jopo la madaktari waliomfanyia uchunguzi wa akili yake, iliyoeleza kuwa wakati wa tukio hilo hakuwa na akili timamu.
Wakati Rama akiachiwa kwa kutokana na ripoti hiyo ya madaktari, mama yake aliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka (Jamhuri) katika kesi hiyo namba 26 ya mwaka 2010, kudai kuwa hauna nia ya kuendelea kumshtaki.
Kuachiwa kwa washtakiwa hao kulisababisha vilio kwa mama wa mtoto aliyeuawa, Upendo Dustani na shangazi wa mtoto huyo, Furaha Mussa, aliyekuwa akiishi na mtoto huyo nyumbani kwake Tabata.
Septemba 29, 2011, Mahakama Kuu iliamuru Rama apelekwe katika hospitali ya magonjwa ya akili ili apimwe akili kama alikuwa na akili timamu au la, wakati wa tukio hilo.
Amri hiyo ya Mahakama iliyotolewa na Jaji Samuel Karua, ilitokana na maombi yaliyotolewa na Wakili Yusuph Shehe aliyekuwa akiwatetea
Wakili Shehe alisema ameamua kutoa ombi hilo ili kujiridhisha na utimamu wa akili za mshtakiwa kwanza kabla ya kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo kulingana na kumbukumbu za maelezo ya ushahidi ulioko mahakamani.
Jana, kabla ya washtakiwa hao kuachiwa, Wakili wa Serikali, Secy Mkonongo aliyekuwa akisaidiana na Clara Charles, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali, kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao.
Hata hivyo Wakili Shehe alidai kuwa mara ya mwisho Mahakama hiyo iliamuru mshtakiwa wa kwanza, Rama, apelekwe katika hospitali ya magonjwa ya akili kwa ajili ya uchunguzi wa akili yake.
Wakili Shehe alisema ripoti hiyo tayari imeshawasilishwa mahakamani hapo kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Akili Isanga tangu Juni 20, 2012, ikiwa imesainiwa na Dk Mndeme Erasmus na kwamba inaeleza kwa mshtakiwa wakati akitenda kosa hilo hakuwa na akili timamu.
“Kutokana na ripoti hii, ninaiomba Mahakama yako ijielekeze katika vifungu cha 220 (4) na 219 (2) vya CPA kinachoelekeza Mahakama.
 akili wa Serikali Mkonongo alisema kuwa upande wa mashtaka hauna pingamizi.
Akitoa uamuzi, wake Jaji Rose Temba alisema kuwa Mahakama imetilia maanani ripoti hiyo kuwa ya uchunguzi wa akili za mshtakiwa wa kwanza kuwa wakati akitenda tukio hilo hakuwa na akili timamu.
Jaji Temba alisema kuwa kwa mujibu wa ushahidi ulitolewa mahakamani hapo, inaamini kuwa mshtakiwa wa kwanza alitenda kosa la mauaji.
Hata hivyo alisema kuwa kulingana na ripoti hiyo ya daktari kuwa mshtakiwa hakuwa na akili timamu, chini ya kifungu cha 219 (2) CPA, Sura ya 20 kama kilivyorekebishwa mwaka 2002, Mahakama haiwezi kumtia hatiani.
“Naamuru aendelee kubakia chini ya uchunguzi wa Watalamu wa magonjwa ya akili na hospitali itakuwa ikitoa taarifa kwa Waziri wa Sheria na Katiba.”, alisema Jaji Temba.
Baada ya uamuzi huo dhidi ya Rama, Wakili wa Serikali, Mkonongo alisema katika kesi hiyo walibakiwa na mshtakiwa mmoja, mama yake Rama, lakini akasema kutokana na uamuzi upande wa mashtaka hauna nia ya kuendelea kumshtaki.
Awali Wakili Mkonongo aliwasomea washtakiwa hao mashtaka na maelezo ya mashtaka yanayowakabili ambapo alidai kuwa April 25, 2008, saa 2:30 usiku, mtoto Salome alikuwa akicheza nje ya nyumba ya Shangazi yake Furaha Majani, akiwa na Rama na mwenzao Paschael.
Alisema baada ya baba wa mtoto huyo Yohana Mussa Majani alifika kwa dada yake huyo na kumkuta mkewe, akauliza kwa nini walikuwa wamemwacha mtoto yule nje hadi wakati ule? Wakili Mkonongo alidai kuwa Furaha alipotoka nje hakumkuta, lakini Paschael akawaambia kuwa alikuwa amepotea katika mazingira tata na kwamba aliwaambia wazazi wake wakamtafuta.

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595