Ijumaa, 12 Aprili 2013

SHEIKH: WAKRISTO WANAYO HAKI YA KUCHINJA


SHEIKH wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhadi Mussa Salum, amezungumzia mzozo wa kuchinja na kusema kuwa muumini wa dini yoyote anahaki ya kuchinja. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sheikh Salumu, alisema suala la kuchinja kila mtu anaweza kuchinja kutokana na imani yake.

Alhad alisema muumini wa dhehebu lolote anaweza kuchinja, huku akitoa angalizo kuwa uchinjaji huo uzingatie imani ya watumiaji wa nyama hiyo.

Sheikh Alhad alisema kwamba Wakristo wana haki ya kuchinja ilimradi nyama hiyo ni kwa ajili ya matumizi yao wenyewe katika familia zao na si vinginevyo.

“Binafsi sina tatizo katika suala la kuchinja kwani kulingana na utamaduni tuliokuwa nao Wakristo wana haki ya kuchinja kwa matumizi yao wenyewe na kama ni kwa ajili ya matumizi ya umma basi Waislamu wafanye hivyo,”alisema.

Aidha alizidi kusisitiza kuwa suala la kuchinja linahitaji mjadala miongoni mwa viongozi wa dini wenywewe na si kuitupia lawama Serikali kwa kuibua mijadala ambayo ni vigumu kwa Serikali kuwa na majibu yake kwa wepesi zaidi.

Alisema Serikali haiwezi kusuluhisha tatizo hilo bali ni kusimamia utatuzi wake, hivyo viongozi wa dini wana wajibu wa kuandaa mijadala yenye lengo la kuweka sawa mambo hayo.

“Kwa kupitia mijadala hii itakayo waunganisha viongozi wa dini zote mbili, wananchi wataweza kupata ukweli wa mambo mbalimbali yanayoonekana kuwa kero na yanayohatarisha ustawi wa amani ya nchi yetu.

“Sote ni wadau wa amani hivyo ni wajibu wetu sisi viongozi wa dini kukaa na kuzungumzia matatizo yaliyopo ili tuweze kurejesha amani ambayo kwa sasa inatetereka ,”alisema Sheikh Salum

0 comments:

Chapisha Maoni

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595