Hukumu ya Sheikh Ponda yaahirishwa hadi Mei Tisa
Hakimu Mkazi Alocye Katemana ndiye aliyeairisha kesi hiyo ambapo alianza kwa kusema kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya kutolewa hukumu, lakini hukumu hiyo haitatolewa kwa sababu hakimu anayesikiliza kesi hiyo hayupo na wala hajatuma hukumu ya kesi hiyo kwa uongozi wa mahakama.
“Kwa sababu hiyo naairisha kesi hii hadi Mei 2 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na Mei 9 mwaka huu, itakuja kwa ajili ya kutolewa hukumu...”
Alisema Hakimu Katemana na kuamuru mshitakiwa wa kwanza na watano (Ponda na Mukadam Swalehe) kurudishwa rumande kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Dk Elizer Feleshi hajaondoa hati yake ya kuwafungia dhamana.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alifika mahakamani hapo tangu saa moja asubuhi, alishuhudia kundi la watu zaidi ya mia moja wakiwa wamesimama nje ya uzio wa mahakama hiyo karibu na ofisi ya Maktaba ya Taifa tayari wakisubiri kuingia ndani ya lango la mahakama hiyo kwa ajili ya kukaguliwa kwa vifaa maalum na wanausalama.
Watu hao waliruhusiwa kuingia ndani ya viwanja vya mahakama, lakini ni wachache tu ndiyo walioruhusiwa kuingia ndani ya chumba cha wazi Na.2 cha mahakama hiyo kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.
Baada ya kuarishwa kwa kesi hiyo, askari magreza waliondoka na msafara wa magari yao ambao ulikuwa ukiongozwa na askari polisi waliokuwa wamevalia na wasiovalia sare za jeshi.
Wakati wakitoka ndani ya viwanja hivyo tayari kuelekea katika gereza la Segerea anapoishi Ponda na Mukadam kwa sasa, wafuasi hao walipaza sauti huku wakimpungia mkono Ponda wakisema ‘Takbir!’ na kuitikia ‘Allahu Akbar.’
0 comments:
Chapisha Maoni