Jumatatu, 8 Aprili 2013

HATIMAYE KESI YA MAUAJI YA PADRI ALIYEUAWA KULE ZANZIBAR YAANZA

Mtuhumiwa wa mauaji ya Padri Evaristus Mushi, Omar Mussa Makame (35) mkazi wa Mwanakwerekwe mjini hapa amefikishwa Mahakama Kuu kwa tuhuma za mauaji ya kiongozi huyo wa dini.
Makame aliyegombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Rahaleo mwaka 2010 alifikishwa mbele ya Jaji Mkusa Sepetu jana.
Awali mtuhumiwa huyo alikuwa afikishwe mahakamani Jumanne iliyopita, lakini ilishindikana baada ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Zanzibar kuinyima kibali Polisi kumfikisha mahakamani.
Haikujulikana sababu ya uamuzi huo kwani Mkurugenzi wa Mashtaka, Ibrahim Mzee Ibrahim na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa walitupiana mpira kila mmoja akitaka mwenzake ndiye ataje sababu hizo.
Viongozi hao wote jana hawakupatikana kueleza hatua hii mpya ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo imekuja baada ya uamuzi wa aina gani.
Wakili wa Serikali, Abdallah Issa Mgongo alidai mbele ya Jaji Sepetu kuwa mshtakiwa aliua kwa makusudi Februari 17, mwaka huu eneo la Beit el Rass Wilaya ya Magharibi Zanzibar.
Mgongo alidai tendo hilo ni kosa kwa mujibu wa vifungu 196 na 197 sheria namba (6) za mwaka 2004 ya sheria za Zanzibar.
“Omar Mussa Makame unashitakiwa kwa kosa la kumuua kwa makusudi Padre Evarist Mushi siku ya tarehe 17/02/2013 mnamo saa 12:50 za asubuhi,” alidai Wakili Mgongo.
Makame alikataa kosa hilo la mauaji na wakili wa Serikali aliiomba Mahakama kumrudisha rumande mtuhumiwa hadi hapo ushahidi utakapokamilika.
Upande wa utetezi wakili wa kujitegemea, Abdallah Juma aliiomba Mahakama iamuru ushahidi ukamilike baada ya wiki mbili ili kesi iweze kusikilizwa.
“Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa ni kwamba ushahidi umekamilika nashangaa leo (jana) wakili wa Serikali anasema kwamba bado haujakamilika,” alidai Juma.
Baada ya maombi hayo, Jaji Sepetu alikubaliana na upande wa utetezi na kuwataka mawakili wa Serikali kuharakisha kupeleka ushahidi ili kesi ianze kusikilizwa. Kesi hiyo imepangwa Aprili 18, mwaka huu katika mahakama hiyo.

0 comments:

Chapisha Maoni

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595