Mamia ya watu wanahofiwa kuuawa au kujeruhiwa baada ya tetemeko kubwa la
ardhi leo nchini China karibu na mji wa Ya'an kusini-magharibi mwa
jimbo la Sichuan.
Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.6 kwenye kipimo cha Richter, na ambalo
kiini chake kilikuwa umbali wa km 13 chini ya ardhi limetokea mapema leo
asubuhi katika eneo la Lushan, karibu na eneo lilipotokea tetemeko
jingine mwaka 2008 na kuwaua zaidi ya watu 85,000.
Awali idara ya tetemeko la ardhi ya China, ilitangaza kuwa tetemeko hilo
la ardhi lilikuwa na ukubwa wa 7.0 kwenye kipimo cha Richter, lakini
idara ya utafiti wa jiolojia ya Marekani ikaweka sawa kipimo hicho na
kutangaza kuwa ni cha 6.6.
Shirika la habari la China-Xinhua, limethibitisha kuwa watu 20 wamekufa
hadi sasa na wengine zaidi ya 400 wamejeruhiwa, wanne kati yao wakiwa
katika hali mbaya, huku taarifa zikieleza kuwa idadi hiyo inaweza
ikaongezeka.
Matetemeko yalisikika katika mji wa Chongping eneo wanapoishi kiasi watu
milioni 30. Xinhua imeonyesha picha za wakaazi hao wakiwa nje za nyumba
zao baada kusikia mitikisiko.
Likimnukuu mkaazi wa Chengdu, Xinhua, limesema kuwa mkaazi huyo
aliona mitikisiko kwa sekunde 20 na baada ya hapo aliona kuta za nyumba
ya jirani zikaanza kubomoka.
Wanajeshi wapelekwa kutoa msaada
Kwa mujibu wa Xinhua, kiasi wanajeshi 2,000 wamepelekwa katika eneo hilo
kwa ajili ya kutoa msaada katika zoezi la uokozi. Ofisi ya majanga na
tetemeko la ardhi ya Sichuan, imesema kuwa miji kadhaa imelisikia
tetemeko hilo, ambalo limetikisa sana majengo ya mji mkuu wa jimbo hilo,
Chengdu.
Uwanja wa ndege ulifungwa kutokana na tetemeko hilo, kabla ya
kufunguliwa tena saa moja baadaye. Timu mbalimbali za uokozi zimeelekea
katika eneo hilo la Chengdu kwa ajili ya kutoa msaada na taarifa
zinaeleza kuwa Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao ameelekea pia katika
eneo la tukio.
Wakaazi wa eneo hilo wanaotumia mitandao ya kijamii, wamesema kuwa
tetemeko hilo limekata huduma za umeme na maji. Mwaka 2008 eneo hilo
lilikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.9 katika
kipimo cha Richter na kusababisha vifo vya watu 90,000, kujeruhiwa
maelfu pamoja na kufanya uharibifu mkubwa wa mali katika eneo hilo.
0 comments:
Chapisha Maoni