JUKWAA LA WA WAKRISTO TANZANIA (TCF)
“ATUKUZWE MUNGU JUU MBINGUNI, NA DUNIANI IWE AMANI KWA WATU ALIOWARIDHIA” (Lk.2:14)
TAMKO LA PAMOJA LA MKUTANO MKUU WA DHARURA WA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA
1.Utangulizi
Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) linajumuisha Taasisi Kuu za Makanisa nchini kama ifuatavyo:-
Jumuiya ya Kikristo Tanzania – CCT
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania – TEC
Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania – PCT
Kanisa la Waadventisti Wasabato – SDA (Watazamaji)
Katika Mkutano wake Mkuu wa Dharura
uliofanyika katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini, Jijini Dar es Salaam, tarehe 8 Machi,
2013; Wajumbe walitafakari kwa undani juu ya kuzorota kwa mahusiano
baina ya Dini mbili za Ukristo na Uislamu nchini Tanzania, pamoja na
mauaji na mashambulizi ya viongozi wa dini; na hatua zilizochukuliwa na
Serikali dhidi ya uhalifu huo unaotekelezwa na Waislamu wachache. Katika
taswira hiyo, Kanisa lilitathmini juu ya wajibu, utume, na sauti yake
ya kinabii kwa taifa letu kuhusiana na mambo hayo.
2. Hali halisi ilivyo hivi sasa hapa nchini kwa mtazamo wa Kanisa
Ushahidi
wa kihistoria na kimazingira unaonyesha wazi kuwa kwa sasa Kanisa
nchini Tanzania limo katika kipindi cha mateso ya kimfumo (systematic
persecution), kama vipindi vingine 10 vya mateso katika Historia ya
Kanisa hapa duniani. Pamoja na mateso haya ya kimfumo, tunatambua wazi
kuwa wanaotekeleza haya ni kikundi kidogo tu cha Waislamu wa Tanzania,
kama wale wengine wa Barani Afrika (k.m. Boko Haram kule Nigeria).
Waislamu walio wengi hawafurahii mambo yanayotokea. Wao pia wanaitazamia
Serikali kuthibiti hawa wachache wanaochafua dini ya Kiislamu na
kuwafanya Waislamu wote waonekane kuwa maadui wa Ukristo, jambo ambalo
siyo kweli.
Kutokana na hali hiyo, mkutano mkuu wa
dharura wa Jukwaa la Wakristo umeyaangalia maeneo makuu yenye migogoro
ikiwa ni pamoja na:
2.1. Mgororo wa nani anastahili kuchinja kitoweo Hivi karibuni hapa
nchini tumeshuhuduia mgogoro juu ya uchinjaji wa mifugo ambayo nyama
yake inapaswa kuuzwa kwa watu wa imani mbalimbali wakiwemo Wakristo na
Waislamu. Tunafahamu kwamba sheria ya nchi yetu inaweka bayana juu ya
usalama wa nyama hizo kiafya, lakini sheria haielekezi kuwa dini fulani
ndiyo waumini wake wanapaswa kuchinja mifugo hiyo. Kwa misingi hiyo
Kanisa linatamka kuwa:-
a) Hoja ya dini moja kudai kuhodhi (exclusive right) uchinjaji wa mifugo
kwa misingi ya imani yake ni kinyume cha haki ya uhuru wa kuabudu
ambayo amepewa kila mtu ndani ya nchi hii kikatiba katika Ibara 19.
b)
Kwa kuwa kuchinja wanyama na ndege ni Ibada kwa Waislamu, Kanisa
litambue na kuheshimu jambo hilo. Lakini pamoja na kutambua haki ya
Waislamu kujichinjia wanyama na ndege kama Ibada kwao, Wakristo
wasilazimishwe kula nyama zilizochinjwa kwa misingi ya Ibada za
Kiislamu. Kwa kuwa wananchi wa Tanzania ni wa dini mbalimbali na mila za
makabila mbalimbali, tunaitaka Serikali itamke wazi kuwa kila raia ana
uhuru wa kufuata imani yake katika suala la uchinjaji.
c) Kuhusiana na jambo hili tunashindwa
kabisa kuelewa msimamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Viongozi wengine waandamizi wa Serikali. Wakati wa Serikali ya awamu ya
pili chini ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ambaye pia ni Muislamu,
ulipotokea ugomvi wa mabucha ya nyama ya nguruwe Dar es Salaam, Rais
huyu Mstaafu kwa kulinda Katiba ya nchi ambayo aliapa kuilinda, alisema
mwenyewe kwa nguvu zote kuwa kila mtu ana uhuru wa kula anachotaka na
mtu wa dini moja asimhukumu mtu wa dini nyingine kwa kile anachokula.
Baada ya Rais Mstaafu kukemea jambo hili, hali ikawa ya amani na
utulivu. Kwa nini Serikali yetu ya sasa inapata kigugumizi kuhusiana na
suala zima la nani achinje?
d) Kwa mantiki hiyo hapo juu katika
kipengele cha a-c, Wakristo wanaitaka Serikali iweke utaratibu wa
kugawana machinjio na mabucha kati ya Wakristo na Waislamu ili kila
Mtanzania awe huru kujinunulia kitoweo mahali anapotaka. Sambamba na
kuitaka Serikali kufanya hivyo, tunawakumbusha Wakristo wote Tanzania
kuelewa kuwa watakuwa hawajavunja sheria yoyote ya nchi wakiamua
kujichinjia kitoweo chao wenyewe. Kuhusiana na tangazo hili kwa Wakristo
wote, tunaitaka mihimili ya dola (Serikali na Mahakama) kuheshimu
Katiba ya Nchi yetu, na kipekee kuhusiana na jambo hili Ibara ile ya 19.
e) Kwa upande mwingine, kwa kuwa
tayari zipo bidhaa za vyakula katika nchi hii ambazo zina nembo ya
‘halal’ na nyingine hazina nembo hiyo, huu ni uthibitisho kuwa vyakula
hivyo vimegawanywa kwa kufuata misingi ya imani za kidini. Kwa hiyo,
madai ya kugawanya machinjio na mabucha kwa kufuata misingi ya dini sio
jambo jipya kwa sasa katika nchi hii.
2.2 Uchomaji wa Makanisa ulioambatana na
vitisho na mauaji ya viongozi wa KanisaKanisa linalaani vikali mauaji ya
kidini yanayoendelea kufanywa pamoja na vitisho (systematic
persecution) kwa viongozi wa Kanisa na Wakristo wote kwa ujumla.
Mtiririko wa matukio mbali mbali ya
nyuma yanatudhihirishia kuwa kumekuwepo na mpango wa muda mrefu wa haya
yanayotokea sasa hivi. Tarehe 15 Januari 2011, kundi la Waumini wa
Kiislamu walipokutana katika ukumbi wa Diamond Jubilee, miongoni mwao
walikuwamo mashehe, walijadili hali ya nchi ya Tanzania kuongozwa kwa
mfumo wa kidini. Mkutano huo ulihitimishwa kwa kutoa tamko dhidi ya kile
kilichoitwa mfumo Kristo katika nchi yetu!
Japo Serikali na vyombo vyake vya
usalama wa Taifa vimekuwa vikipata taarifa za vitisho dhidi ya viongozi
wa Kanisa, mauaji, kuchomwa kwa nyumba za ibada, pamoja na maneno ya
uchochezi kupitia mihadhara, vipeperushi, CD na vyombo vya habari
vinavyomilikiwa na taasisi zinazofahamika, hata hivyo Serikali kwa kiasi
kikubwa imeshindwa kuchukua hatua kwa wakati muafaka na wanasubiri hadi
maovu yatendeke ndipo ati waanze kufanya uchunguzi. Kwa Serikali yetu
inaonekana wazi kuwa katika hili ile methali kwamba “Kinga ni bora
kuliko tiba” haina maana yoyote. Hii ni kuonyesha udhaifu mkubwa wa
vyombo vya usalama wa Taifa au pia kwamba vyombo hivi vinafurahia
kutoweka kwa amani nchini mwetu, jambo ambalo linalifanya Kanisa nchini
Tanzania liamini kwamba matukio haya yanayoendelea kutokea ni dalili
kuwa Serikali ina agenda ya siri dhidi ya Ukristo.
Kutokana na hayo Jukwaa la Wakristo Tanzania linatamka kama ifuatavyo:
a) Tunatambua kwamba ni jukumu la Serikali kuwatendea raia wake kwa
usawa na bila ya ubaguzi kwa mujibu wa Ibara ya 12 na 13 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Viongozi wa Kanisa wanatamka kwamba
Serikali imeshindwa kuheshimu Katiba juu ya hizi haki za raia wake na
kupelekea waamini wa dini ya Kikristo kukosa imani na Serikali iliyoko
madarakani, hasa kuhusu ulinzi na usalama wao na mali zao kama
inavyoagizwa kwenye Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania. Kama Serikali inaona haiwezi kuwahakikishia wananchi usalama
wa uhai wao na mali zao, na hivyo kuwafanya waishi maisha ya hofu
inayotokana na vitisho, basi kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, hakuna
sababu ya Serikali iliyoko madarakani kung’ang’ania kuongoza nchi.
b)
Kwa kuwa ulinzi wa raia ni haki ya kikatiba na kisheria, Serikali
inatakiwa iwalinde raia wake. Kama Serikali imeshindwa kuwalinda raia
wake, Kanisa linataka Serikali ikiri hivyo ili Kanisa liwaambie wananchi
waiwajibishe Serikali na Viongozi wanaoifanya Serikali ishindwe
kutimiza wajibu wake.
Jukwaa la Wakristo linasema:
Kama Serikali haitachukua hatua za makusudi dhidi ya mambo haya
yaliyoainishwa hapo juu, Kanisa litachukua hatua ya kuwaambia waamini
wake kwamba Serikali iliyoko madarakani inaibeba dini moja, na hivyo
Kanisa litatafakari upya uhusiano wake na Serikali.
3. Wakristo walioko Zanzibar
Wakristo walioko Zanzibar wanatishiwa maisha yao na mali zao
zinaharibiwa mara kwa mara, kiasi cha wengine kuamua kuhamia Tanzania
Bara. Kigezo cha unyanyasaji huo ni suala la udini na muungano.
Inaonekana ni kama vile Watanzania waliozaliwa Bara hawana haki ya
kuishi Visiwani. Na kumbe wale waliozaliwa Visiwani wafikapo Barani wana
haki zote. Kanisa linaitaka Serikali iwahakikishie Wakristo walioko
Zanzibar usalama wao na wa mali zao maana hiyo ni haki yao ya Kikatiba.
4. Vitisho na mauaji ya Wanakanisa
Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ichukue hatua za makusudi za
kuzuia vitisho na mauaji kwa Viongozi wa Kanisa na Wakristo kwa ujumla.
Vinginevyo Kanisa litautangazia ulimwengu kuwa Tanzania ni nchi
mojawapo inayovunja haki za binadamu kwa ubaguzi wa kidini na kulitesa
Kanisa kimfumo.
5. Matumizi ya Vyombo vya Habari:
Kwa kuwa kuna baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimeruhusu vitumiwe
kuwatukana Viongozi wa Kanisa, tunatoa nafasi kwa vyombo hivyo kuomba
radhi; vinginevyo tutaitaka dunia ivielewe kuwa navyo ni sehemu ya
chanzo cha migogoro. Pia tunachukua nafasi hii kuvitahadharisha vyombo
mbalimbali vya habari kupima kwa kina ni nini kinachosemwa na viongozi
wa kidini ili kuviepusha vyombo hivyo kutumika kwa nia ya uchochezi;
yasije yakatukuta kama yale yaliyotokea kule Rwanda 1994.
6. Hitimisho:
Kanisa linaendelea kusisitiza kuwa silaha kuu ya Mkristo katika nyakati
hizi ni maombi na kufunga. Kwa mantiki hiyo, Kanisa linawataka Wakristo
wote nchini Tanzania kuungana kwa pamoja katika maombi na kufunga kwa
muda wa siku saba kwa ajili ya hali hii iliyojitokeza hapa nchini.
Maombi hayo na mfungo vifanyike kabla ya Pasaka, yaani kuanzia, tarehe 24/3/2013 hadi 30/3/2013.
Kwa niaba ya Maaskofu 177 walioshiriki katika Mkutano Mkuu wa Dharura wa Jukwaa la Wakristo na kutoa maazimio hayo.
1. Askofu Peter Kitula – Mwenyekiti CCT
2. Askofu Tarcisius J. M. Ngalalekumtwa Rais TEC
3. Askofu David Batenzi Mwenyekiti PCT
0 comments:
Chapisha Maoni