Alhamisi, 30 Mei 2013

LIPUMBA AREKODIWA KATIKA VIDEO AKIHAMASISHA UDINI!!

 
 BAADA YA KUSOMA HABARI HII TUNAOMBA UCHANGIE MAWAZO YAKO NA MTAZAMO WAKO JUU YA VIDEO HII ILIYOREKODIWA
 
Mwishoni mwa wiki zilipatikana taarifa za kushitua kumhusu Mwenyekiti wa Taifa cha Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba. Gazeti moja liliripoti kuwa limenasa mkanda wa video unaomwonyesha Prof. Lipumba si tu akikiri kuwa alimsaidia Rais Jakaya Kikwete kupata ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita bali pia ‘akihamasisha udini’ kwa kutaka Waislamu wajipange kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Awali nilitarajia mambo mawili, kwanza, Profesa Lipumba kupata ujasiri wa kufafanua kuhusu video hiyo, na pili, taarifa kutoka Ikulu aidha kukanusha au kufafanua kuhusu ‘msaada wa Prof Lipumba kwa Rais Kikwete.’ Hadi ninapoandika makala hii, hayo yote hayajatokea, na hivyo kilichozungumzwa na Lipumba kinaendelea kubaki halali.
Ni vema tutakumbuka kuwa hivi majuzi tu, Rais Kikwete alieleza bayana kuwa kuibuka kwa tatizo la udini kuna ‘mkono wa nchi za nje.’ Binafsi, nilitafsiri kauli hiyo ya Rais kama ‘kutoa majibu mepesi kwenye maswali magumu.’ Ninapata taabu kuamini maelezo ya Rais wangu kuhusu uhusika wa mataifa ya nje kwenye tatizo la udini hususan kwa sababu hakutaja japo nchi moja inayochochea tatizo hilo huko nyumbani.
Na kwa upande mwingine, kutaja tu uhusika wa mataifa ya nje hakutoi maelezo ya kutosha kwani bado kuna swali la; je, ni sera ya taifa fulani dhidi yetu au ni vitendo vya watu binafsi walio nje ya nchi dhidi ya taifa letu.’
Ukisikiliza kwa makini maelezo ya Prof Lipumba, unaweza kuelewa vyema jinsi udini ulivyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambapo Kikwete aliibuka mshindi. Lipumba amebainisha wazi kwenye video hiyo kuwa Waislamu walihamasishwa kumpigia kura Kikwete kwa matarajio kwamba angesaidia kutatua matatizo yao. Hata hivyo, kwa mujibu wa video hiyo, inaelekea kuwa matarajio hayo hayajatimia, na Lipumba amesikika akihamasisha Waislamu “Wajipange kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015...kwa vile wenzetu (ninaamini akimaanisha Wakristo) wameshaanza kujipanga.”
Katika namna isiyopendeza kabisa, Prof Lipumba amejaribu kuifanya ajenda ya utajiri wa rasilimali tulionao, ambao unahujumiwa na mafisadi, kuwa ina uhusiano na ‘wenzetu’ (yaani Wakristo).
Nilitarajia Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, angekuwa mtu wa kwanza kutoa wito kwa Lipumba kuachia ngazi mara moja, kama ambavyo amekuwa ‘mwiba mkali’ kwa CHADEMA kiasi cha kujengeka picha kuwa Msajili huyo ni mithili ya mtumishi wa CCM.
Pamoja na ‘kumhukumu’ Prof. Lipumba kwa kauli zake, binafsi ninaamini kuwa alizungumza hayo si kama Mwenyekiti wa CUF bali muumini tu wa kawaida wa dini ya Kiislamu. Tatizo ni kwamba ni vigumu kutofautisha matamshi ya Lipumba mwanasiasa na Lipumba muumini. Lakini kibaya zaidi, bila kujali matamshi hayo yalitolewa na Lipumba katika wadhifa gani, madhara yake yanabaki kuwa makubwa.
Hivi tukiweka kando mkanda huo mmoja wa video, Prof Lipumba ameshapita katika misikiti mingapi akimwaga sumu hiyo ya udini? Je, Lipumba anaweza kuwathibitishia Watanzania kuwa kuna chama kimoja (ambapo ni dhahiri alimaanisha CHADEMA) kinafanya harakati za kuingia Ikulu kwa kusaidia na mataifa yasiyoutakia mema Uislamu?
Wakati hoja za mwanasiasa huyo msomi kuhusu jinsi nchi yetu ilivyo tajiri wa rasilimali lakini inakwamishwa na ufisadi unaolelewa na CCM zina mashiko, ‘tiba’ anayopendekeza ya kutumia udini si tiba bali ni sumu kali kabisa.
Ningependa kuchambua kwa undani zaidi kuhusu suala hili lakini nafasi hainiruhusu. Hata hivyo, ninaomba kuhitimisha makala hii kwa kutoa wito wa haraka kuwa Profesa Lipumba anastahili kujiuzulu mara moja.
Kauli zake za kuchochea udini hazina nafasi hata kidogo katika siasa za Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa tatizo la udini limeshasababisha madhara kadhaa hadi sasa.
Kwa Lipumba kuendelea kubaki madarakani itarejesha picha ile ile ya mwaka 1995 kwamba CUF inatumia Uislamu kama silaha yake ya kisiasa, kwani haiwezekani chama kuwa chini ya Mwenyekiti anayehubiri udini pasipo chama hicho kuridhia udini kuwa ni moja ya sera zake.
Iwapo Lipumba atagoma kujiuzulu, basi ninaisihi CHADEMA (ambayo japo haikutajwa bayana kwenye video hiyo) ianzishe jitihada za kuhakikisha mwanasiasa huyo ‘anakwenda na maji.’
Kadhalika, ninataraji Msajili wa Vyama vya Siasa, Tendwa atatumia nguvu ile ile anayotumia dhidi ya CHADEMA kuchukua hatua stahili dhidi ya Prof Lipumba.
Vilevile, iwapo Lipumba hatojiuzulu, ninashauri waumini wa dini ya Kikristo kumshinikiza Lipumba ajiuzulu kwa sababu kamwe hatuwezi kuruhusu kuwepo kwa Uchaguzi Mkuu ambao mmoja wa wagombea urais (labda Lipumba atagombea tena mwaka 2015) ni mdini (angalau kwa mtizamo wake).
Nihitimishe makala hii kwa kutoa wito wa moja kwa moja kwa Profesa Lipumba kuwa licha ya kuthamini mchango wake kwa taifa na kimataifa, hususan katika nyanja za siasa na uchumi, alichokizungumza hakikubaliki hata kidogo. Na ni matarajio yangu kuwa atakuwa muungwana kwa sio tu kuomba radhi Watanzania pasi kujali itikadi zao za kisiasa na kidini, bali pia kujiuzulu uenyekiti wa CUF mara moja.
 Kwa wale wanaotaka kuangalia video angalia link hii http://www.chahali.com/2013/05/lipumba-arekodiwa-kwenye-video.html

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595