Siku zote tunaamini kuwa mtu anapofariki hupumzika kwa amani, lakini siku hizi wafu hao hawapumziki tena kwa amani, bali huamshwa, kisha, wafu wengine kushika nafasi zao.
Ni kama vile muda wa marehemu hao kukaa kaburini
umekwisha hivyo, nafasi zao zinatakiwa kutumiwa na wengine kutokana na
uhaba wa maeneo ya kuzikia.
Maeneo mengi ya kuzikia katika Jiji la Dar es
Salaam, hasa yale maarufu kama Kinondoni, Sinza, Temeke na Kisutu
yanapendwa zaidi na watu na sasa yamefurika.
Kujaa kwa maeneo haya ya kuzikia kumesababisha makaburi ya watu wengine, kufukuliwa kisha kutumika kuzikia miili mingine.
Hata hivyo, makaburi ambayo hufukuliwa ni yale
ambayo hayajajengewa, yametelekezwa, hayana kitu chochote cha kuonyesha
kuwa kuna kaburi pale au mengine hayana alama kama misalaba au
imeondolewa.
Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian
Kaiohela anasema kuwa anafahamu kwamba makaburi hayo yamejaa, lakini
hakutaka kuzungumza zaidi akitoa ahadi kuwa siku ya Jumatatu
atalifikisha suala hilo kwa wahusika wakuu.
Katika makaburi ya Temeke Chang’ombe, Mwananchi
Jumapili lilishuhudia makaburi yakiwa yamesongamana kiasi ambacho ni
vigumu mtu kupata nafasi ya kuweka mguu.
Mlinzi wa makaburi hayo, Athuman Mtembwe anasema
kutokana na ufinyu wa nafasi katika makaburi hayo, makaburi ambayo
hayana alama yoyote ni rahisi kufukuliwa na kuzikiwa kwa mara nyingine.
“Mimi kama mlinzi wa eneo hili ninaweza
kukutafutia sehemu ambayo unaweza kuchimba kaburi, lakini kama hufahamu
utafukua tu maiti nyingine,” anasema
Anasema kuwa mara kwa mara watu wanaokuja kuchimba
makaburi ili kuzika ndugu zao, wamekuwa wakifukua miili ya watu wengine
ambayo makaburi yao hayakuwa na alama yoyote.
“Ni kawaida, mchimba kaburi anafukua, anakuta
mifupa, anaiweka pembeni au anaizika katika shimo dogo…kisha anaendelea
na taratibu za kuzika mwili mwingine,” anaeleza.
Lakini Mtembwe anasisitiza kuwa iwapo atachimba
yeye, hawezi kufukua kaburi lililokwishatumika kwani anafahamu maeneo
machache ambayo hayajatumika, ingawa ni finyu mno.
0 comments:
Chapisha Maoni