Jeshi la ulinzi wa amani la Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo limetishia kutumia nguvu za kijeshi kuwazuia waasi
kusonga mbele kuukaribia mji wa Goma baada ya kuzuka mapigano makali
mapya.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imesema watu 130, wakiwemo
wanajeshi wake 10 wameuwawa katika mapigano hayo mapya yaliyohusisha
jeshi lake na waasi wa M23 ambayo yametokea katika viunga vya mji wa
Goma kwa upande wa mashariki hapo jana.Katika wiki za hivi karibuni Umoja wa Mataifa umewasilisha kiasi ya wanajeshi 3,000 madhubuti wa ulinzi wa amani huko mashariki mwa Kongo. Jeshi la pamoja linaloundwa na askari kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi kwa mara ya kwanza kabisa limepewa nguvu na baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuweza kutumia nguvu dhidi ya makundi ya waasi.
Tahadhari kwa waasi yatolewa.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky amesema tayari jeshi hilo limewekwa katika hali ya tahadhari na kuwa tayari kuchukua hatua zozote muhimu zikijumuisha kutumia silaha kali kwa lengo la kuwalinda raia. Msemaji huyo ameongeza kwa kusema jaribio lolote la kuukaribia mji wa Goma litachukuliwa kama kitisho cha moja kwa moja kwa raia.
Kwa mujibu wa kikosi maalum la ulinzi wa amani cha Umoja wa Mataifa katika eneo hilo la Kivu ya Kaskazini MONISCO mapigano ya hivi karibuni yalizuka eneo la Mutaho, umbali wa kiasi cha kilometa tano kaskazini/magharibi mwa mji wa Goma.
Aidha MONUSCO imesema kuwa waasi wa M23, ambao wana nguvu za kutosha katika baadhi ya maeneo Goma, wanadhibiti maeneo yao kwa kutumia silaha nzito. waasi wa M23 ambao wataalam wa Umoja wa Mataifa wanasema wanapata uungwaji mkono kutoka Rwanda na Uganda Novemba mwaka uliyopita waliuteka mji wa Goma na kuchochea Umoja wa Mataifa kufanya jitihada za kusaidia hali ya usalama eneo hilo ambalo mamilioni ya watu wamepoteza maisha kutokana na kugubikwa na mapigano kwa zaidi miongo miwili.
Rwanda yalalamika kushambuliwa.
Katika hatua nyingine msemaji wa jeshi la Rwanda, Joseph Nzabamwita amesema makombora mawili yamefyatuliwa hapo jana kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Msemaji huyo ametupa lawama kwa jeshi la Kongo na MONUSCO kwa kitendo hicho ambapo hata hivyo hakuna yeyote aliejeruhiwa kufuatia mkasa huo.
Katika taarifa yake Nzabamwita amevitaja vijiji vya Kageshi na Gasiza vilivyopo katika wilaya ya Rubavu huko kaskazini/mashariki mwa Rwanda ambavyo vimepakata na eneo tete la mashariki ya Kongo kuwa ndivyo vilivyokumbwa na kadhia hiyo.
Aidha ameliita shambulizi hilo kuwa ni kitendo cha makusudi na kichokozi katika maeneo hayo ambayo hakuna mapigano yoyote kwa hivi karibuni baina ya makundi hasimu. Wakati huo huo Rwanda imeituhumu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa kushirikiana na waasi wa Kihutu FDLR, ambao kiongozi wao anatafautwa kwa tuhuma ya kuhusika na mauaji ya Kimbari ya 1994.
0 comments:
Chapisha Maoni