Jumanne, 9 Julai 2013

CHADEMA YAJIPANGA KAMA KIJESHI

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kuanza kujihami kwa kuboresha kikosi chake cha ulinzi na usalama cha Red Brigade, kwa kutoa mafunzo maalumu ya ukakamavu yatakayoandaliwa katika makambi maalumu yaliyosambazwa katika mikoa yote nchini.

Pamoja na hilo, kimetangaza kuanza kuanika uozo wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mataifa yote duniani, kwa kuchapisha kitabu maalumu kitakachosambazwa ili kuonyesha namna wanavyotendewa matendo ya kikatili na kuuawa huku serikali ikiendelea kukaa kimya.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana kwa dharura kwa muda wa siku mbili Julai 6 na 7 mwaka huu.

Alisema kutokana na matukio ya kigaidi na mengine ya ukiukwaji wa haki za binadamu aliyodai kuwa yanafanywa na baadhi ya viongozi wa serikali pamoja na wa CCM, sasa umefika wakati wa kuchukua hatua badala ya kuendelea kulia.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kukisuka upya kikosi cha Red Brigade, kwa kukipa mafunzo upya ambayo ni maalumu kwa ajili ya kujihami.

Mbowe alisema kikosi hicho kitakuwa na shughuli maalumu ya kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya wagombea, wanachama na viongozi wa Chadema.

Alisema uamuzi huo umefikiwa na Kamati Kuu ya Chadema, baada ya Jeshi la Polisi kuonekana kuwa haliwajibiki ipasavyo.

“Kikosi hiki kilionekana kulegalega ndio maana tumeendelea kukumbwa na matukio ya kikatili namna hii.

“Tukiendelea kulia tutakuwa wajinga, kwa sababu Jeshi la Polisi ndilo linaloshirikiana na CCM sasa umefika wakati tutaandaa makambi maalumu kwa ajili ya mafunzo hayo,” alisema.

Wakati Mbowe akitangaza uamuzi huo, kumekuwa na hofu kutokana na matendo yanayodaiwa kufanywa nyuma ya vikosi hivyo vinavyomilikiwa na vyama mbalimbali nchini.

Vikosi hivyo, ni pamoja na Red Brigade kinachomilikiwa na Chadema, Green Guard kinachomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi na Blue Guard cha CUF.

Vikosi hivyo mara nyingi vimekuwa vikidaiwa kujifua kijeshi na hata kupatiwa mafunzo wanayopatiwa watu wa usalama, ambayo huyatumia kutekeleza vitendo vya kijangili.

Wakati Chadema ikitangaza hadharani kuhusu uamuzi wake huo wa kukinoa kikosi chake, mwezi mmoja uliopita chama hicho mkoani Mbeya kilikishutumu CCM kwa kuanzisha kambi zinazoendesha mafunzo ya kijeshi.

Baadhi ya wachambuzi na wafuatiliaji wa siasa za hapa nchini, wanasema kuwa vikosi vya kujihami kama hivyo vimechangia uvunjifu wa amani hapa nchini hususani nyakati za uchaguzi.

Jinai inayodaiwa kutendwa na vikosi hivyo, ni kugusa maeneo mbalimbali.

Baadhi ya matukio kama kuteka watu, kuua, kumwagiwa tindikali na mengine mengi, baadhi yake yamekuwa yakidaiwa kutekelezwa chini ya vikosi hivyo.

Hata hivyo licha ya CCM kuwa ya kwanza kutajwa na jambo hilo kuzungumzwa hadharani mara kadhaa, baadhi ya wachambuzi na wafuatiliaji wa masuala ya siasa wanaona kuwa vyombo vya dola havijachukua hatua stahili na sasa ugonjwa huo umeambukiza vyama vingine ambavyo awali havikuwa na utaratibu huo.

KUHUSU KITABU CHENYE USHAHIDI

Akizungumzia azma yao ya kuchapisha kitabu maalumu ambacho kitaanika uozo unaofanywa dhidi yao na Serikali ya chama tawala, Mbowe alisema:

“Tumetengeneza ‘compilation’ au kitabu maalumu ambacho kitaonesha matukio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyofanywa na viongozi wa Serikali na CCM na kukifikisha kwa mataifa yote, serikalini na kwa wananchi ili kuonesha ulimwengu kama matukio haya yanafanywa na Chadema au CCM wenyewe,” alisema.

Mbowe alisema, kutokana na ugaidi pamoja na vitendo vingine vya unyanyasaji vinavyofanywa na serikali kiujumla, aliwahi kumtaka Rais Kikwete aunde tume huru ya kimahakama ili kuchunguza matukio hayo likiwamo lile la Arusha, ila hadi sasa ameendelea kukaa kimya.

“Kwa maana hiyo sisi tutaendelea na msimamo wetu ule ule wa kutotoa ushahidi wowote kwa Jeshi la Polisi, kwa sababu baadhi yao ndio wanaoshiriki kulipua mabomu hayo kwa kushirikiana na CCM.

“Iwapo Rais ataendeleza msimamo wa kutounda tume huru ya kimahakama, ushahidi uliopo juu ya tukio la kurushwa bomu Arusha utawekwa wazi muda utakapofika kwa wananchi wa Tanzania pamoja na jumuiya ya kimataifa, ili yaishinikize serikali kuunda tume huru ya kimahakama kuchunguza shambulio hilo na matukio mengine yenye sura ya kisiasa,” alisema.

Alisema kitabu hicho maalumu kinatarajiwa kukamilishwa hivi karibuni na kuanza kusambazwa ili kuishinikiza serikali ichukue hatua, kwani kuendelea kukaa kimya na kulia pekee hakuna maana.

Kwa mujibu wa Mbowe hadi sasa wanachama zaidi ya 2,000 wa chama hicho wamekamatwa na kufunguliwa mashitaka mbalimbali ya kubambikizwa nchi nzima, huku akidai kuwa matukio yote yanafanywa na serikali kwa kupitia CCM na Jeshi la Polisi.

Pamoja na hilo, Mbowe alisema Kamati Kuu imelaani kitendo cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi cha kudanganya bunge kuwa Chadema ndiyo waliojirushia bomu wenyewe.

“Kauli hii ya Lukuvi ni ya kitoto, kijinga na kiwendawazimu, kwa sababu haiwezekani sisi wenyewe tutake kujiua kwa kujiongezea umaarufu, hatutafuti umaarufu kwa njia hizo za kigaidi,” alisema.

Kuhusu msimamo wa chama hicho kwenye Rasimu ya Katiba mpya, Mbowe alisema tayari wameandaa kitabu maalumu kitakachochambua na kuelezea msimamo wake kuhusu rasimu hiyo.

Alisema kitabu hicho kitazinduliwa katika mkutano wa hadhara ambao utatangazwa siku chache zijazo.

0 comments:

Chapisha Maoni

Call Us Now:

+255 655 732121, +255 716 758595 / +255 762 758595