Vikosi vya uokoaji vinasema, watu wapatao 30
wamefariki dunia na mamia wengine wanahofiwa kukwama baada ya jingo la
ghorofa nane kuporomoka katika mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka.
Juhudi za ziada zinaendelea kuwaokoa watu
walionaswa kwenye kifusi. Watu wapatao 200 wamejeruhiwa kufuatia ajali
hiyo. Jeshi linasaidia shughuli za uokoaji katika eneo la tukio nje
kidogo ya jiji la Dhaka.Jengo lililoporomoka lilikuwa na kiwanda cha nguo, benki na maduka kadhaa. Liliporomoka asubuhi wakati watu wakielekea makazini.
Watu wengi wamekusanyika karibu na eneo la tukio wakiwatafuta ndugu na marafiki. Mwandishi wa BBC mjini Dhaka anasema haijafahamika kilichosababisha jengo hilo kuporomoka, lakini vyombo vya habari nchini humo vimearifu kwamba, nyufa zilionekana kwenye jengo hilo siku ya Jumanne.
Polisi wameviambia vyombo vya habari kwamba, waliona ghafla sehemu ya nyuma ya jengo hilo ikianguka Jumatano asubuhi na baada ya muda mfupi jengo lote likafuatia isipokua nguzo kuu na sehemu ya ukuta wa mbele hali iliyosababisha taharuki.
Maafisa wanasema, ni sehemu ya chini pekee ya jengo hilo la Rana Plaza ndio ilibakia imara baada ya kuporomoka, wakati wanajeshi na waokoaji wa idara ya zimamoto wakiwa na vifaa vya kukatia vyuma na matingatinga wakifukua kifusi ili kuwaokoa watu walionaswa .
Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Mohammed Asaduzzaman, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, hali ilikua mbaya sana.
Novemba mwaka jana, moto uliounguza kiwanda cha nguo nje ya jiji la Dhaka uliua watu 110 na kusababisha wananchi kupigia kelele kuhusu viwango vya usalama kwenye viwanda husika.
Mara mwisho jengo la ghorofa nne liliporomoka jijini Dhaka mnamo mwaka 2010 na kusababisha vifo vya watu 25 na wengine kadhaa kujeruhiwa.
0 comments:
Chapisha Maoni